Wadau wa vyama vya siasa watakiwa kutambua umuhimu wa daftari la kudumu
21 October 2021, 12:15 pm
Na Said Abdalla:
Mwenyekiti wa tume ya uchaguzi Zanzibar Jaji mkuu mstaafu Hamid Mahmoud Hamid amesema ni utamaduni uliojengwa na tume ya uchaguzi wa kukutana na wadau wake kila inapotokea jambo linalohusu uchaguzi.
Ameyasema hayo kwenye mkutano wa wadau wa uchaguzi kuhusu uwekaji wazi orodha za wapiga kura wanaotaka kuhamisha taarifa na waliopoteza sifa za kuwa wapiga kura katika Ukumbi wa mkutano wa Makonyo Wawi Chakechake Pemba
Amesema Baada ya kukamilika kwa uchaguzi mkuu wa Zanzibar mwaka 2020, tume ya uchaguzi imeendelea na hatua za uendelezaji wa daftari la kudumu la wapiga kura kwa kupokea maombi ya wapiga kura wanaoomba kuhamisha taarifa zao kutoka eneo moja la kupigia kura na kwenda katika eneo jengine.
Amesema Tume ya uchaguzi ya Zanzibar inakusudia kufanya kazi ya kuhamisha taarifa za wapiga kura walio wasilisha maombi yao na kuwafuta wapiga kura waliopoteza sifa za kuwa wapiga kura ili kuliweka daftari la kudumu katika hali ya usahihi.
Amewataka wadau wa uchaguzi kuwahamasisha wananchi itakapofika tarehe 25/10/2021 kwenda katika ofisi za tume za wilaya zilizoandaliwa na tume kwa lengo la kujiridhisha kutokana na majina yaliyo bandikwa ili waweze kujuwa kuwa ni wapiga kura sahihi.
Amesema kuwa Tume ya uchaguzi ya Zanzibar haitomfuta mpiga kura yeyote katika daftari la kudumu la wapiga kura mpaka pale itakapopokea taarifa sahihi na ya kujiridhisha kupitia mamlaka zinazohusika au jamaa wa karibu wa muhusika.
Ameongeza kuwa sharia ya uchaguzi ya Zanzibar kifungu cha 4 (1) (c) imeipa jukumu tume ya uchaguzi ya Zanzibar kuandaa, kutayarisha, kuhifadhi na kuendeleza daftari la kudumu la wapiga kura.
Amewataka wananchi kudumisha Amani na utulivu, na kutoa ushirikiano kwa shughuli zinazoendeshwa na tume ya uchaguzi ya Zanzibar katika mzunguko wote wa uchaguzi.
Akitoa maelezo juu ya utaratibu wa kuweka wazi orodha za wapiga kura walipoteza na wanaotaka kuhamisha taarifa zao, Mkurugenzi wa uchaguzi Khamis Kombo Khamis amesema sharia ya uchaguzi ya Zanzibar kifungu cha 32, inamtaka Afisa uandikishaji kutayarisha na kuweka wazi orodha ya wapiga kura waliohamisha taarifa zao au kupoteza sifa za kuwa wapiga kura kwa siku 7.