FIFA watoa mafunzo kwa walimu wa michezo Ngorongoro
7 April 2024, 2:21 pm
Mafunzo ya ukocha ngazi ya awali kwa walimu wa michezo shule za msingi na sekondari yameanza kitolewa wilayani hapa ambapo moja ya faida kubwa ambazo wanufaika wataipata na kuelewa na kufahamu zaidi mbinu mbalimbali za mpira wa miguu na mifumo yake.
Na Mwandishi wetu.
Walimu wa michezo wilaya ya Ngorongoro wameanza rasmi mafunzo ya ukocha wa mpira wa miguu kwa ngazi ya awali (grassroot) April 6, 2024 katika uwanja wa Loliondo sekondari ambapo mafunzo hayo yametolewa na mwakilishi kutoka Shirikisho la Mpira wa Miguu Duniani (FIFA) kupitia Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF).
Mafunzo hayo yamesimamiwa na afisa michezo wilaya ya Ngorongoro Ndg, Ngoka Simon na yatatolewa kwa muda wa siku tano kisha vyeti vitatolewa kwa walimu wote watakao hitimu mafunzo hayo.
Akizungumza wakati wa mafunzo hayo katika mafunzo hayo uwanja wa Loliondo sekondari ndg, Ngoka amesema lengo la mafunzo hayo ni kuwandaa vyema walimu wanaokwenda kuwafundisha watoto mpira wa miguu shuleni ili kuboresha taaluma ya michezo wilaya ya Ngorongoro.
Akizungumza kwa niaba ya walimu wa michezo wa shule za sekondari na msingi mwl. Grace Luka amesema wameyapokea vyema mafunzo hayo kwani yatakwenda kuwanufaisha wao walimu, wanafunzi ambao ni walengwa na kuimarisha vipaji vya watoto na hata kuiweka wilaya ya Ngorongoro katika ramani ya michezo.
Jumla ya walimu wa michezo 27 wa shule za sekondari na msingi wameshiriki mafuzo hayo na yanatarajiwa kufika ukomo mnamo tarehe 10 Aprili, 2024 huku serikali ikiendelea kulipa nafasi suala la michezo katika sekta ya elimu kwa kuanzia ngazi ya shule za msingi na sekondari.