Loliondo FM

Walimu FC mabingwa Ngorongoro

30 September 2025, 1:01 pm

Picha ya kikosi cha walimu fc wakiwa kwenye picha ya pamoja kabla ya mchezo wa ligi ya wilaya ya Ngorongoro (picha na Zacharia James).

Ligi ya mpira wa miguu wilaya ya Ngorongoro imetatamatika licha ya kukumbwa na changamoto kadha wa kadha ikiwepo kukosekana kwa bajeti ya kutosha kuendesha ligi hiyo.

Na mwandishi wetu.

Walimu FC wametawazwa mabingwa wa Ligi ya Wilaya ya Ngorongoro baada ya kuibuka na ushindi kwa mikwaju ya penalti dhidi ya Olosokwan FC katika fainali iliyopigwa mwishoni mwa wiki kwenye uwanja wa shule ya sekondari ya Loliondo.

Mchezo huo uliochwezwa Septemba 28,2025 ulimalizika kwa sare ya bao 1–1 ndani ya dakika 90 na kuamuliwa kwa mikwaju ya penalti ambapo Walimu fc walipiga kwa umakini mkubwa na kushinda kwa penalti 4 -2.

Awali, Olosokwan walitangulia kupata bao kupitia Moondo Terta kwa shuti kali la mbali, lakini Walimu FC walisawazisha kupitia Onesmo Ole Kurduni kwa mpira wa faulo.

Katika mchezo wa kutafuta mshindi wa tatu, Soitsambu fc waliibuka kidedea baada ya kuichapa Loliondo Sports bao moja kwa sifuri.

Hata hivyo fainali ilifuatiwa na utuaji wa tuzo kwa waliofanya vizuri kwenye ligi ambapo Gift Gervas alichaguliwa kuwa mchezaji bora wa mashindano, huku Frugence Augustino wa Walimu FC akitwaa tuzo ya kipa bora huku chipukizi bora akiibuka kuwa Lucas Juma wa Soitsambu fc,timu yenye nidhamu ikawa Oldonyowas fc na kwa upande wa wafungaji bora, Izack Jacob wa Walimu fc alifungana na Moondo Terra wa Ololoswakwan fc na Bariki Simon wa Soitsambu fc, kila mmoja akifunga mabao matatu.

Hata hivyo chama cha mpira wa miguu wilaya ya Ngorongoro NGODIFA kupitia ripoti ya mashindano kimewapongeza mabingwa wa ligi kwa ujumla pamoja na timu shiriki zote kwa kuonyesha ushindani na nidhamu wakati wote wa mashindano.