Loliondo FM
Loliondo FM
16 May 2025, 4:35 pm

Viongozi na watendaji mbalimbali wa kiserikali hapa nchini wamekuwa wakitoa matamko ya kumpongeza rais wa jamhuri ya muungano wa Tanzania Dr Samia Suluhu Hassan kwa maendeleo wanayoataja wao yameletwa nae.
Na Zacharia James
Baraza la madiwani halmashauri Ngorongoro limepitisha azimio lakumpongeza rais wa jamhuri ya muungano wa Tanzania Mhe.Dr Samia suluhu Hassan kwa kuunda tume mbili za kushughulikia migogoro ndani ya wilaya ya Ngorongoro.
Azimio hilo limepitishwa Alhamisi ya Mei 15, 2025 Katika kikao cha baraza la madiwani wa halmashauri ya wilaya ya Ngorongoro kujadili utendaji wa halmashauri katika kipindi cha robo ya tatu ya mwaka wa fedha 2025.
Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Ngorongoro Mhe. Marekani Mohamed bayo amemshukuru rais Dk Samia kwa kuunda tume kwaajili ya kufuatilia migogoro maeneo ya Loliondo,pori tengefu la Pololet,natron na eneo la tarafa ya Ngorongoro ili kutatua kero na changamoto za wananchi na hatimaye kumaliza migogoro mingi iliyopo wilaya ya Ngorongoro.
Mkuu wa wilaya ya Ngorongoro Mhe.kanali Wilson sakulo wakati akizungumza kupitia baraza hilo ameshukuru na kusifu jitihada za rais wa jamhuri ya muungano wa Tanzania kwa kuwezesha miradi mingi ya maendeleo na kiwasihi madiwani na wataalam kufanya kazi kama timu na kwa bidii ili kuwaletea wananchi maendeleo.
Kwa upande wake mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Ngorongoro Murtallah Sadiki Mbilu amebainisha mkakati wa pamoja ukihusisha kamati ya usalama wilaya,wataalam wa halmashauri pamoja na madiwani ili kufuatilia namna gani halmashauri ya wilaya ya Ngorongoro itaweza kunufaika ipasavyo na mapato makubwa yatokanayo na rasilimali zinazopatikana ikiwemo mapato yatokanayo na shughuli za uhifadhi katika eneo la mamlaka ya hifadhi ya Ngorongoro (NCAA).
Awali diwani wa kata ya Arashi Mhe.Methiew Silooma aliyetowa hoja hio ameungana na diwani wa Engaresero Ibrahim Sakai na Mhe.Agmeli Kalamban aliewakilisha madiwani wanawake kumshukuru rais kwa kuunda tume hizi ambapo mbali na mambo mengine wameitaja hatua hiyo kama ya matumaini na kuponya majeraha ya muda mrefu ya wananchi wa jamii za kifugaji wilayani hapa kukosa maeneo ya malisho na maji kwaajili ya mifugo na ardhi ya kutosha kwa shughuli nyingine za kijamii ikiwemo kilimo.