Loliondo FM

Dkt. Chana aipongeza hifadhi ya Ngorongoro kukusanya zaidi ya bilioni 96

16 October 2024, 11:30 pm

Balozi Dkt Pindi Chana waziri wa maliasili na utalii katikati akiongoza kikao na menejimenti ya mamlaka ya hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) picha na mpiga picha.

Waziri wa maliasili na utalii mh balozi dkt Pindi Chana amekuwa akifanya vikao mara kwa mara na mamlaka ya hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) kwa lengo la kujenga mahusiano mazuri baina ya wizara, NCCA na wananchi waishio pembezoni wa hifadhi ya Ngorongoro.

Na mwandishi wetu.

Waziri wa maliasili na talii mh balozi dkt Pindi Chana amezitaka taasisi zilizoko chini ya wizara ya maliasili na utalii kufanya kazi kwa kushirikiana ili kuboresha utendaji kazi wa taasisi hizo.

Balozi Chana ametoa kauli hiyo leo Oktoba 16,2024 wakati akizungumza na menejimenti ya mamlaka ya hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) katika kikao kilichofanyika jengo la kitega uchumi la Ngorongoro jijini Arusha.

Amesisitiza kuwa kama kuna huduma ambazo zinatolewa na taasisi mojawapo zilizopo ndani ya wizara hiyo ni muhimu kushirikiana ili kurahisisha utendaji kazi na hivyo kuongeza ufanisi katika utendaji katika sekta ya uhifadhi na utalii.

“Fuateni sheria na taratibu zilizopo ili kuongeza ushirikiano wa taasisi zote, nawasisitiza pia kujenga utamaduni wa kutembeleana kwa lengo la kujifunza, na kama kuna uwezekano wa kusaidiana vifaa vya kufanyia kazi katika maeneo mbalimbali saidianeni ili kuondoa changamoto katika taasisi fanyeni hivyo .” amesema waziri Chana.

Aidha, balozi dkt Pindi Chana imeipongeza mamlaka ya hifadhi ya Ngorongo kwa kuweza kukusanya jumla ya shilingi bilioni 96.7 katika robo ya kwanza ya mwaka 2024/25 ukilinganisha na robo ya kwanza ya mwaka wa fedha 2023/2024 ambapo mamlaka hiyo ilikusanya shilingi bilioni 68.

Kwa upande wake kamishna wa uhifadhi wa mamlaka ya hifadhi ya Ngorongoro dkt Elirehema Doriye alimweleza eaziri Chana kwamba mamlaka inaendelea kutekeleza majukumu yake kwa umakini ili kuhakikisha kuwa inafikia malengo iliyojiwekea ya kuboresha shughuli za uhifadhi na kuongeza idadi ya watalii ili kufikia malengo yaliyowekwa na serikali.

Mhe. Chana yupo jijini Arusha kutembeleza taasisi mbalimbali zinazosimamiwa na wizara ya maliasili na utalii ambapo ameongozana na naibu katibu mkuu (Utalii) Bw. Nkoba Mabula pamoja na mkurugenzi wa utalii Dkt.Thereza Mugobi.