FCS, NGOLAC waahidi kushirikiana kusaidia jamii
16 September 2024, 10:56 am
Katika kuhakikisha inaendelea kuboresha huduma za kijamii taasisi ya NGOLAC imeendelea kukutana na wadau mbalimbali ili kuimarisha utoaji wa huduma kwa jamii kwa kushirikiana na wadau hao.
Na Saitoti Saringe
Akizungumza Septemba 15/2024 katika ofisi za NGOLAC zilizopo ofisi za halmashauri ya wilaya ya Ngorongoro Bw. Dani Fayo kutoka FCS amesema kuwa lengo la kukutana na taasisi hiyo ni kuona ni namna gani wanavyoweza kufanya kazi na NGOLAC kulinda haki za watumiaji wa bidhaa mbalimbali katika maeneo ya Biashara, Mawasiliano pamoja na Usafiri.
Aidha Bw Dani Fayo amesema kuwa wanalenga pia kuwajengea uwezo wafanyakazi wa shirika hilo namna ya kulinda haki za watumiaji wa bidhaa mbalimbali kisha waweze kuwafikishia wananchi wa jamii za kisonjo na kimasai namna ya kuzitambua haki zao katika matumizi ya bidhaa hizo.
Ngorongoro Legal Aid Center (NGOLAC) ni kituo kinachotoa huduma za msaada wa kisheria za kupambana na ukatili, msaada kwa walemavu pamoja na masuala ya mazingira.
Mpaka hivi sasa ni mwaka mmoja tangu NGOLAC ianze kazi zake katika wilaya ya Ngorongoro ambapo imefanikiwa kuwafikia zaidi ya walemavu 200 na kutoa huduma mbalimbali kama vile Elimu, fimbo nyeupe kwa walemavu lakini vile vile taasisi hii kwa mwaka mmoja tu imefanikiwa kufanya kazi na wadau wa nje na ndani ya nchi ili kuweza kusaidia kufikisha huduma kwa jamii.