Aliyetoroka na kwenda Msomera kwa kulazimishwa kuolewa arejea Ngorongoro
20 June 2024, 8:12 pm
Mwanamke huyo anasema alitolewa mahari akiwa darasa la pili na mwanaume ambaye alihitaji kumuoa baada ya binti huyo kuhitImu kidato cha nne lakini binti huyo hakuwa tayari kuolewa na mwanaume huyo licha ya kuishi naye kwa muda mchache na kuambulia kipigo pamoja na manyanyaso kutoka kwa mwanaume huyo.
Na Edward Shao.
Binti mmoja mkazi wa kijiji cha Sendui kata ya Alailiai tarafa ya Ngorongoro mwenye umri wa miaka 21 aliyelazimishwa kuolewa na mwanaume asiye chaguo lake awasili ofisi za ustawi wa jamii wilaya ya Ngorongoro kutokea Msomera Tanga.
Akizungumza katika ofisi za ustawi wa jamii Bi Felis Namingi afisa ustawi wa jamii wilaya ya Ngorongoro amekiri kumpokea binti huyo (24) leo Juni 20,2024 majira ya saa nne asubuhi akiwa na kesi ya unyanyasaji na ndoa ya kulazimishwa.
Amesema binti huyo alipomaliza kidato cha nne wazazi wake walimlazimisha kuolewa licha ya kufaulu kwenda vyuo vya kati lakini alilazimishwa kuolewa na mwanaume mwenye umri wa miaka 41 hali iliyompelekea binti huyo kutoroka na kwenda Msomera Tanga.
Binti huyo ameeleza baada ya kulazimishwa kuolewa amekumbwa na vitendo vya unyanyasaji ikiwepo kubakwa, vipigo na kunyimwa matumizi na mahitaji ya msingi hali iliyomfanya yeye kutoroka na kwenda kwa mjomba wake aliyeko Msomera.
Kwa upande wake mratibu wa watu wenye ulemavu kupitia kituo cha msaada wa kisheria Ngorongoro Bw. Moses Mollel kwa kushirikiana na ofisi ya ustawi wa jamii na kumpokea binti huyo ameiasa jamii kuachana na vitendo vya kikatili na kuviripoti katika kituo cha msaada wa kisheria kwani kituo hicho kipo kwa ajili ya watu wote na siyo wanawake na watoto pekee na hata wanaume.
Jamii za kifugaji batemi na masaii zinazopatikana wilayani Ngorongoro zimekuwa zikishikilia mila zilizopitwa na wakati ikiwemo ndoa za utotoni na ndoa za lazima huku wakitoa adhabu kali kama vile vipigo kwa wanawake wanaogoma kuolewa kwa lazima na kusababishia madhara kwa wanawake hao ikiwepo kifo.