Frankfurt yatoa ufadhili wa ufundi stadi Ngorongoro
23 May 2024, 6:49 pm
Shirika la Frankfurt zoological society ni moja ya mashirika yasiyo ya kiserikali ambapo makao makuu yake yapo katika mji wa Frankfurt nchini Ujerumani likiwa linajishughulisha na huifadhi wa mazingira ya asili na viumbe hai katika mazingira ya asili huku likifanya kazi na serikali ya jamhuri ya muungano wa Tanzania kupitia wizara ya maliasili na utalii.
Na Edward Shao.
Shirika la Frankfurt lazindua mpango wa kusaidia vijana kujipatia ujuzi wa kuweza kupata ajira kupitia mafunzo ya chuo cha ufundi stadi VETA.
Akizungumza hii leo Mei 23,2024 katika katika hafla hiyo ya uzinduzi wa mradi huo iliyofanyika katika ukumbi wa mikutano wa chuo cha ufundi stadi cha wilaya ya Ngorongoro mgeni rasmi na mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Ngorongoro mh Marekani Bayo amewahasa wanafunzi 30 waliopata nafasi ya ufadhili kutumia fursa hiyo vizuri na kushikana mkono pale mmoja wao atakapokuwa anakata tamaa yakuendelea kusoma.
Naye mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Ngorongoro bwn Murtallah Sadiki amesema wanafunzi hao watakapohitimu mafunzo yao,miradi ya maendeleo ya halmashauri kama itahitaji wataalam basi watapewa kipaumbele wahitimu hao katika kuitekeleza.
Kwa upande wake ndg, Masegeri Rurai meneja miradi shirika la Frankfurt amesema lengo la mradi huo ni kusaidia vijana wa kike na wakiume katika wilaya ya Ngorongoro kutoka katika tarafa za Loliondo na Sale kujiunga na chuo cha VETA kujipatia ujuzi na hatimaye kujiajiri au kuajiriwa katika fani mbalimbali za ufundi.
Amesema kuwa kwa mwaka huu wamesadia vijana wapatao 30 kwa kushirikiana na hifadhi ya taifa (TANAPA) kupitia kitengo cha ujirani mwema na ufadhili wa benki ya maendeleo ya Ujerumani (KFW) huku wakitumia zaidi ya milioni 35 kwa vijana hao kupata mafunzo kwa muda wa miaka 2 kuanzia mwaka 2024 hadi 2025.
Sambamba na hayo shirika hilo limewalipia wanafunzi wote 30 ada na kuwapatia mabegi, daftari,kalamu,tishert na mahitaji mengine huku wale wanafunzi wa kutwa wakipatiwa kila mmoja shilingi 3000 kila siku kwa mahitaji yao binafsi kama vile nauli yakwenda chuoni na kurudi nyumbani.
Mmoja wa wanafunzi wanufaika wa ufadhili huo Lengume Shakwa amelishukuru shirika la Frankfurt zoological society pamoja na serikali kwa ujumla kwa kufanikisha mafunzo kwao huku akiahaidi kusoma kwa bidii.
Wanafunzi hao 30 wanufaika wa mradi huu katika awamu hii ya kwanza ni kutoka katika vijiji vya Sakala,Ololosokwan,Mageri,Eyasi,Mdito,Sakala,Lopuluni,Soiti sambu,Sukenya,Olorien,Piyaya,Orkuyaine ambao wanapata mafunzo ya ufundi wa kushona,umeme na uashi katika chuo cha ufundi stadi cha wilaya ya Ngorongoro.