Wananchi Samunge, Digodigo kero zao mikononi mwa Dc Sakulo
15 March 2024, 12:36 pm
Ni muendelezo wa zira za mkuu wa wilaya Kanali Sakulo katika kutembelea vijiji na kata mbalimbali kusikiliza na kutatua kero za wananchi.
Na mwandishi wetu
Wananchi Kata ya Samunge na Kata ya Digodigo Machi 14, 2024 wamemshukuru Mhe. Mkuu wa Wilaya ya Ngorongoro Kanali Wilson Sakulo kwa ziara yake ya kuwatembelea, kusikiliza na kutatua kero. Pia wamejitokeza kwa wingi ili kumsikiliza na kutoa kero zao katika Mkutano wa hadhara uliotishwa na Mkuu wa Wilaya kisha kuonyesha kuvutiwa na njia hiyo aliyotumia Mhe. Mkuu wa Wilaya ya kuwasikiliza wananchi wake.
“Kwanza naipongeza Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kutuletea miradi mingi, kwa kipindi cha miaka mitatu tumeletewa miradi yenye thamani ya bilion 1.2, ikiwemo Barabara, Shule pamoja na mradi wa umwagiliaji pia kwa kutuletea Mkuu wa Wilaya unayejali watu unaowaongoza tunashukuru sana”-Mhe. Baraka Diwani wa Digodigo
Akizungumza katika Mkutano huo Bi. Beti Meriedi Mkazi wa Kijiji cha Mdito kata ya Samunge amemshukuru Mkuu wa Wilaya kwa ujio wake na kuitisha Mkutano ili Wananchi wenye kero na matatizo wapate msaada, amesema jambo hilo linawatia faraja.
” Mhe. Mkuu wa Wilaya tunashukuru kwa ujio wako ili wenye matatizo na wenye kero wapate msaada tunakushukuru sana na karibu Samunge”-Bi. Beti Meried
Hata hivyo wakati wa hotuba yake Mhe. Kanali Wilson Sakulo ametoa rai kwa Wananchi wa Digodigo na Samunge kutanua fikra zao katika upande wa maendeleo kwa kukubali wawekezaji wanapojitojeza katika maeneo yao kwaajili uwekezaji, kwani ndio chachu ya maendeleo ya Kata zao na Taifa kwa ujumla.
Mhe. Kanali Sakulo ameongeza kwa kusema kuwa Soko jipya la Wasso limeanza kutumika kwa shughuli za kuhudumia jamii katika upande wa mahitaji muhimu kama vyakula na nguo ambapo sehemu ya mnada kuanzia ijumaa ya tarehe 15 Machi utakua katika viunga vya Soko jipya hivyo wasisite kwenda kufanya biashara zao pale, kwa maana maeneo yapo ya kutosha na kila mfanyabiashara atapata eneo bila shida.
Aidha Mkuu wa Wilaya ametoa agizo kwa Uongozi wa Kata ya Digodigo watenge eneo maalumu kwaajili ya Soko kwa watu wa Digodigo amesema hayo wakati anajibu kero ya Wananchi wa Digodigo ya kutokua na sehemu maalumu ya Soko.
“Lazima tuwe na eneo la Soko hapa Digodigo nikirudi hapa nataka nikute Wananchi wamepata Soko la linatumika”ameongeza Kanali Sakulo
Kwa upande wakeKaimu Mkurugenzi wa TAKUKURU Bw. Godwin Mrutwa ametoa elimu kwa Wananchi hao kupinga na kuzikataa njia za rushwa na kutoa taarifa pindi wanaposhuhudia au kuombwa rushwa na mtumishi yoyote wa umma kisha kutoa namba zake za simu ili pindi tukio lolote la rushwa linapotokea waweze kutoa taarifa haraka.
“Mapambano dhidi ya rushwa niyakwetu wote, uonapo vitendo vya rushwa toa taarifa kwenye Ofisi yoyote ya Umma au kwenye Uongozi wa kata, kijiji au Ofisi ya Mkurugenzi sisi tutalishughulikia, na hata ukiona TAKUKURU awawajibiki ipasavyo msisite kusema fikeni ofisini, piga simu au tuma ujumbe wa maandishi sisi tutalishughulikia wote waliyohusika”
Wakati wa Mkutano huo Mkuu wa Polisi Wilaya ya Ngorongoro Alphonce Bandia ametumia fursa kuwaasa Wananchi wanatumia vyombo vya moto kuwa na leseni, na wanaomiliki vyombo hivyo vya moto wahakikishe wanaajiri watu wenye taaluma ya udereva na wanaomiliki leseni ili kupunguza ajali na matatizo yanayouokea barabarani.
“Wewe unaendesha chombo cha usafiri cha moto hakikisha unamiliki leseni inayokuruhusu kuendesha hicho chombo mkifanya hivyo mtakua salama”-OCD Bandia
Ikumbukwe Kanali Wilson Sakulo, amekua na ziara ya siku tatu ya kufanya Mkutano wa hadhara ili kusikiliza na kutatua changamoto za Wananchi wa Ngorongoro, ambapo ameamua kuambatana na vyombo usalama, Taasisi mbalimbali kama TARURA, TANESCO, RUWASA, TAKUKURU pamoja na Wataalamu wa kutoka Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Ngorongoro ili kuhakikisha changamoto yoyote inayoyolewa na Wananchi utatuzi unalatikana.Pia ziara hiyo imeanza siku ya jumatano ya tarehe 13 Machi 2024.