Nguzo zaanguka Longido, Ngorongoro yakosa umeme
14 March 2024, 3:19 pm
Umeme umeendelea kuwa kero kwa wananchi kutokana na kukosekana kwa huduma hii muhimu kwa shughuli za kila siku kwa kukatika mara kwa mara kwenye maeneo mengi hapa nchini.
Mkuu wa wilaya ya Ngorongoro Mh Kanali Wilson Sakulo tarehe 13 Machi 2024 amefanya mkutano wa adhara katika mji wa Wasso wilayani Ngorongoro lengo likiwa ni kusikiliza na kutatua kero zilizowasilishwa na wananchi kwenye mkutano huo ambapo moja ya changamoto iliyoibuliwa ni kero ya kukatika kwa umeme mara kwa mara.
Akijibu kero hiyo ya kukatika kwa umeme mara kwa mara Kanali Sakulo amesema, kwa upande wa Ngorongoro siyo mgao pekee bali ni changamoto za miundombinu ya umeme kupata shida akitaja miuongoni wa taarifa alizopokea kutoka kwa meneja wa tanesco wilaya ya Ngorongoro ni kuanguka kwa nguzo nne wilayani Longido ambayo imepelekea kukatika kwa umeme wilayani hapa.
Kuhusu swala la kupewa kipaumbele cha mikopo isiyo na riba kwa wafanyabiashara waliohamia katika soko jipya maeneo ya stendi mpya ya mji wa Wasso baada ya wao kutumia fedha nyingi kwenye mchakato wa kuhamisha biashara pamoja na mabanda yao Kanali Sakulo amesema,kwasasa mikopo ya halmashauri zote kwasasa imesimama kwa muda na akiahidi kuwapa kipaumbele mara tu mikopo hiyo itakapoanza kutolewa.