Ngorongoro wahimizwa kuzingatia lishe bora
10 February 2024, 12:27 am
Serikali ya awamu ya sita imeipa kipaumbele sekta ya afya na upande wa lishe ili kuboresha, kuimarisha afya za watoto na kuondoa hali ya udumavu kwa watoto kwa lengo la kuwa na kizazi bora na chenye afya timamu.
Na Edward Shao.
Kuboresha hali ya lishe ili kutokomeza udumavu kwa watoto, leo tarehe 08 Februari 2024 halmashauri ya wilaya ya Ngorongoro imefanya kikao cha tathmini ya utekelezaji wa shughuli za lishe kwa kipindi cha robo ya pili ya mwezi Oktoba hadi Desemba 2023.
Kikao hicho kimehudhuriwa na Bw. Hamza Hamza, Katibu tawala wilaya ya Ngorongoro kama mwenyekiti wa kikao kwa niaba ya mkuu wa wilaya, mkurugenzi mtendaji wa halmashauri Bw. Nassoro Shemzigwa pamoja na wajumbe wengine wa kikao hicho.
Katika kikao hicho Bw. Hamza amewataka watendaji wa vijiji, kata, katibu tarafa kushirikiana na maafisa lishe ili kusaidia katika uboreshaji na kuimarisha hali ya lishe ndani ya wilaya.
Bw. Hamza amesema lengo ni kufanya vizuri kwenye suala zima la lishe hivyo inabidi washirikiane ili waweze kuwa katika hali nzuri ya kiafya na kulinda afya za watoto wao ili kuepukana udumavu.
Kwa upande wake mkurugenzi mtendaji Bw. Nassoro Shemzigwa amesema kuwa ili waweze kuwa na tathmini nzuri ni muhimu kutengeneza utaratibu wa kujipima wao wenyewe.
Amesema lazima wajiwekee malengo kwa kila kipindi ili waweze kujipima wenyewe mbali na mifumo iliyowekwa ili waweze kufanya vizuri kwenye mifumo na katika kipimo cheo wenyewe.
Hata hivyo afisa lishe wilaya Bi. Mariamu Ibrahim amewasilisha taarifa ya tathimini kuanzia mwezi Oktoba hadi Disemba 2023 iliyoonesha ziara za usimamizi shirikishi zimefanyika katika vituo 38 vinavyotoa huduma za mama na mtoto ili kusambaza vitamini A, pamoja na ufuatiliaji wa ubora wa huduma za lishe, jumla ya Watoto 42,172 chini ya miaka mitano walipatiwa matone ya vitamini A.
Aidha taarifa imeonyesha shule 94 zilizopo wilaya ya Ngorongoro zinatoa chakula walau mlo mmoja kwa siku, pia upimaji na utoaji wa elimu ya lishe kwa wanafunzi umefanyika katika Shule 21 zilizotembelewa zenye jumla ya Wanafunzi 1,134 kuanzia darasa la awali na darasa la saba wamefanyiwa uchunguzi wa hali ya lishe ambapo wanafunzi 1,127 sawa asilimia 99 wanahali nzuri ya lishe, huku watoto 7 sawa na asilimia 0.6 walikua na hali mbaya ya lishe na juhudi zilifanyika kuwahudumia watoto hao pamoja na elimu ya lishe bora ilitolewa ili kuepuka matatizo yatokayo na lishe.