Ileje FM

Takukuru yapiga stop wenyeviti vijiji, vitongoji kumiliki mihuri

November 19, 2025, 12:40 pm

Kamanda wa TAKUKURU Wilaya ya Songwe Robert Kahimba akizungumza kwenye mkutano.(Picha na Denis Sinkonde)

Na Denis Sinkonde,Songwe

Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Wilaya ya Songwe imewataka Wenyeviti wa Vitongoji na Vijiji kuacha mara moja tabia ya kumiliki mihuri ya Serikali, ikisema kuwa hatua hiyo ni kinyume cha sheria na imekuwa ikichochea mianya ya rushwa na matumizi mabaya ya madaraka.

Kauli hiyo imetolewa na Kamanda wa TAKUKURU Wilaya ya Songwe Robert Kahimba wakati wa Ziara ya Mkuu wa Wilaya ya Songwe Fadhili Nkurlu aliyoifanya katika Kata za Tarafa ya Songwe hivi Karibuni , ambapo alisisitiza kuwa mihuri ni mali ya Serikali na inapaswa kutunzwa na Watendaji pekee kama ambavyo kanuni za utumishi wa umma zinavyoelekeza.

Kamanda Kahimba aliongeza kuwa Wenyeviti wa Vitongoji na Vijiji ni Viongozi wanaotokana na uwakikishi wa vyama vya siasa hivyo hawana sifa ya kumiliki mihuri ya Serikali .

Sauti ya kamanda wa TAKUKURU Wilaya ya Songwe Robert Kahimba 

Kamanda huyo amesema TAKUKURU imepokea malalamiko kutoka kwa wananchi kuhusu baadhi ya Wenyeviti kutumia mihuri hiyo kutoa nyaraka, vibali na uthibitisho mbalimbali bila kufuata utaratibu, jambo ambalo limesababisha migogoro, upotoshaji wa taarifa na vitendo vya rushwa.

Amesema TAKUKURU itaendelea kufuatilia kwa karibu matumizi ya mihuri katika ngazi za Serikali za vijiji na vitongoji, na yeyote atakayebainika kuendelea kutunza au kutumia mhuri bila mamlaka, atachukuliwa hatua kali za kisheria.

Aidha, TAKUKURU imetoa wito kwa Wananchi kutoa taarifa pindi wanapoona matumizi mabaya ya mihuri, ili kudhibiti mianya ya rushwa na kuhakikisha uwajibikaji unazingatiwa.