Mtegani FM

Serikali yatahadharisha wamiliki boti usalama wa abiria

16 October 2026, 12:18 pm

Picha ikimuonesha Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mheshimiwa Badria Attai Masoud Akiwa katika bandari ya pemba kwenye ziara, Picha na ,Hafsa Ali Idrissa

Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mheshimiwa Badria Attai Masoud, amesisitiza kuwa usalama wa abiria wanaosafiri kwa njia ya bahari ndio kipaumbele kikuu cha serikali na kwamba haitakuwa tayari kusubiri majanga au changamoto zitokee ndipo ichukue hatua.

Na Hafsa Ali Idrissa

Akizungumza wakati wa ziara maalum ya ukaguzi bandarini, Mh. Badria alieleza kuwa ziara hizo zina lengo la kukumbushana na kuhakikisha taratibu zote za usalama zinazingatiwa kikamilifu wakati wote wa safari za vyombo vinavyoelekea Unguja, Pemba, pamoja na Dar es Salaam.

Mheshimiwa Naibu Waziri alibainisha mambo kadhaa muhimu yanayopaswa kuzingatiwa na wamiliki na wasimamizi wa vyombo hivyo, ikiwa ni pamoja na kuhakikisha boti zote zinapakia abiria wanaoendana na uwezo (capacity) halisi wa chombo. Aliongeza kuwa boti zilizoruhusiwa kubeba abiria hazipaswi kuchanganywa na mizigo mikubwa, kwani kitendo hicho kinapunguza ufanisi wa chombo na kuhatarisha usalama wa safari,

Aidha, Mh. Badria alisisitiza uwepo wa vifaa vyote vya usalama ndani ya vyombo, ikiwemo jaketi za kuokoa maisha (life jackets) zinazokidhi idadi ya abiria, pamoja na kuwataka wote wanaojihusisha na usafiri huo kuzingatia kwa umakini taarifa za hali ya hewa zinazotolewa na mamlaka husika,

Mwisho kabisa, alizitaka taasisi zote zinazosimamia masuala ya usafiri na usalama baharini kusimamia sheria na taratibu hizo bila muhali, akionya kuwa serikali haitasita kumchukulia hatua kali za kisheria mtu au taasisi yoyote itakayokiuka miongozo iliyowekwa,

Sauti ya Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mheshimiwa Badria Attai Masoud

Kufuatia ziara hiyo, mwakilishi wa Wizara upande wa Pemba alimshukuru na kumpongeza Mheshimiwa Naibu Waziri kwa hatua hiyo ya ukaguzi, akieleza kuwa taarifa za ongezeko la abiria wengi ziliwalazimu viongozi kujionea wenyewe kama meli zinapakia abiria wakiwa salama

Mwakilishi huyo alimhakikishia Naibu Waziri kuwa wizara upande wa Pemba imeyapokea na kuyabeba maelekezo yote ili kuyasimamia kikamilifu na kuhakikisha boti zote zinabeba abiria kwa viwango vinavyotakiwa, haziondoki wakati hali ya hewa ikiwa mbaya, na kwamba kila chombo kinachofika na kuondoka kinasafiri salama.

Sauti ya mwakilishi wa Wizara upande wa Pemba