Mtegani FM

SUZA yaadhimisha miaka 25 ya mafanikio Zanzibar

7 October 2026, 12:48 pm

Picha ikimuonesha Makamo Mkuu wa Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA), Profesa Said Ali Hamad Vuai, Picha na Hafsa Ali Idrissa.

Makamo Mkuu wa Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA), Profesa Said Ali Hamad Vuai, ametangaza kuanza rasmi kwa maadhimisho ya miaka 25 tangu kuanzishwa kwa chuo hicho, yakilenga kuadhimisha mafanikio ya elimu ya juu, utafiti, ubunifu, na huduma kwa jamii.

Na Hafsa Ali Idrissa

Akizungumza na waandishi wa habari na wadau wa elimu katika mkutano maalum, Profesa Vuai ameeleza kuwa maadhimisho hayo yameanza tarehe 6 Oktoba 2026 na yataendelea hadi mwezi Januari 2027

SUZA ilianzishwa kwa Sheria Namba 8 ya Mwaka 1999 ya Baraza la Wawakilishi la Zanzibar na kuanza masomo rasmi mwezi Septemba 2001 ikiwa na taasisi mbili tu na wanafunzi wachache. Katika kipindi cha robo karne, chuo kimepata mafanikio makubwa kwa kupanua programu zake kutoka 8 pekee mwaka 2010/2011 hadi kufikia programu 66 zilizowasajili zaidi ya wanafunzi 7,000 katika mwaka wa masomo 2025/2026, huku kikizalisha zaidi ya wahitimu 19,000 wanaohudumu katika sekta mbalimbali za maendeleo

Pamoja na mafanikio ya kimasomo, SUZA imeendelea kuimarisha miundombinu yake kupitia miradi mbalimbali kama vile mradi wa HEET uliowezesha ujenzi wa maabara za kisasa, ujenzi wa hosteli mpya mbili zitakazochukua wanafunzi 1,000 kwa ufadhili wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, pamoja na mipango ya ujenzi wa majengo ya utawala, skuli mpya, na viwanja vya michezo kwa ushirikiano na Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB)

Sauti ya Makamo Mkuu wa Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA), Profesa Said Ali Hamad Vuai

Maadhimisho haya yatapambwa na shughuli mbalimbali za kitaaluma na kijamii kama vile mikutano ya habari, kongamano la kitaaluma, maonyesho ya utafiti na ubunifu, michezo, pamoja na huduma za kijamii kama upandaji miti na kambi za afya. Kilele cha maadhimisho hayo kitakuwa Usiku Maalum wa SUZA utakaokwenda sambamba na uzinduzi wa Mfuko wa Kudumu wa Maendeleo (Endowment Fund) kwa ajili ya kujenga Skuli ya Sayansi za Tiba na Hospitali ya Fundishaji (Teaching Hospital). Profesa Vuai ametoa wito kwa serikali, wadau, na jamii kwa ujumla kujitokeza kuunga mkono juhudi hizi za kuijenga SUZA mpya na endelevu.