Mtegani FM
Mtegani FM
1 October 2026, 11:14 am

Rais Mstaafu wa Zanzibar, Mheshimiwa Amani Abeid Karume, akiwa mgeni rasmi, amezindua rasmi uwanja mpya wa michezo wa kisasa uliopo Kitogani, Mkoa wa Kusini Unguja, uliotekelezwa na Wizara ya Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo
Na Hafsa Ali Idrissa
Mradi huo wa daraja la pili, ambao umegharimu dola za Kimarekani milioni 3.2, umejengwa kwa lengo la kukuza sekta ya michezo na kuendeleza vipaji vya vijana na wanamichezo katika ngazi ya mkoa, Ujenzi wa uwanja huo umetekelezwa na kampuni ya Reform Sports Corporation Limited kutoka nchini Uturuki, yenye uzoefu wa kimataifa katika ujenzi wa viwanja vya michezo. Mradi huo umesimamiwa na kampuni ya ushauri elekezi ya wazalendo ya AENQ Company Limited, iliyohakikisha viwango vya ubora vinazingatiwa,

Uwanja huo unajumuisha miundombinu mbalimbali ya kisasa, ikiwemo kiwanja cha kisasa cha mpira wa miguu, jengo lenye vyumba vya wachezaji kubadilishia nguo, huduma za vyoo, ofisi ya msimamizi wa uwanja, na chumba cha huduma ya kwanza. Pia unajumuisha majukwaa ya watazamaji yenye uwezo wa kuchukua watu 500 kwa wakati mmoja, eneo la kimbilio la wanariadha, kiwanja cha matumizi mchanganyiko kwa ajili ya michezo ya mpira wa kikapu, mpira wa wavu, tenisi na mpira wa mikono, pamoja na ukuta wa uzio na eneo maalum la kuegesha (magari).
Wakati wa uzinduzi huo, uongozi wa Mkoa wa Kusini Unguja ukiongozwa na Mkuu wa Mkoa, Hamida Mussa Khamis, pamoja na Mkuu wa Wilaya ya Kusini, Comrade Othman, ulipongezwa kwa ushirikiano wao na wananchi uliowezesha kupatikana kwa eneo hilo na kufanikisha mradi huo hadi kukamilika kwake. Pia shukrani zilitolewa kwa wakandarasi na washauri elekezi kwa usimamizi madhubuti uliowezesha kukamilika kwa uwanja huo kwa viwango vya juu.