Mtegani FM

RC Hamida aagiza maduka yote kufunguliwa saa 3 asubuhi Paje

5 October 2026, 11:36 am

Picha ikionesha Mkuu wa Mkoa wa Kusini Mhe.Hamida Mussa Khamis akizungumza na waandishi wa habari baada ya kukamilika zoezi la usafi wa mazingira katika kijiji cha Paje, picha na Miraji Manzi Kae.

Mkuu wa Mkoa wa Kusini Unguja, Mhe. Hamida Mussa Khamis, amewataka wafanyabiashara na wananchi wa kijiji cha Paje na mkoa mzima kwa ujumla kuimarisha usafi wa mazingira kwa kuagiza maduka yote kufunguliwa kuanzia Saa 3:00 Asubuhi siku za Jumamosi ili kupisha zoezi la usafi linaloanza Saa 12:00 Asubuhi

Na Hafsa Ali Idrissa

Akizungumza mara baada ya kushiriki zoezi hilo lililofanyika kijijini Paje, Mhe. Hamida amebainisha kuwa Mkoa wa Kusini Unguja hivi sasa unakua kwa kasi kubwa katika sekta za utalii na uwekezaji, hivyo ukosefu wa usafi unaweza kukinzana na maendeleo hayo chanya

Aidha, ameyataka Mabaraza ya Mji na Manispaa kuondosha bidhaa, vibanda na magari yote yaliyowekwa pembezoni mwa barabara kwa kuyarudisha nyuma mita 15 ili kupisha huduma nyingine za kijamii, huku akisisitiza kuwa hatua kali za kisheria pamoja na faini zitatozwa kwa yeyote atakayekiuka maagizo hayo

Sauti ya Mkuu wa Mkoa wa Kusini Unguja Mhe. Hamida Mussa Khamis

Wananchi wa kijiji cha Paje walioshiriki zoezi hilo wameipokea kwa mikono miwili kauli hiyo na kuomba zoezi la usafi liwe endelevu. Mwananchi Ali Abass Haji alieleza kuwa Paje ni eneo la kimkakati linalovutia watalii wengi, hivyo usafi wa mara kwa mara utasaidia kuweka taswira nzuri ya kijiji chao

Naye Bi. Asiya Hassan Ally aliongeza kuwa wananchi wenyewe wanapaswa kuwa na utamaduni wa kusafisha mazingira yao na kuondoa taka kama vile chupa za plastiki na nepi bila kusubiri viongozi, hususan katika kipindi hiki ambapo msimu wa mvua unakaribia

Sauti za Wananchi wa kijiji cha Paje wakizungumza baada ya kukamilika kwa zoezi la usafi

Akihitimisha, Mwenyekiti wa Baraza la Mji Kusini, Ndugu Makame Ramadhan Makame, amewasihi wananchi kuendelea kuunga mkono jitihada za viongozi wakuu wa serikali katika kuleta maendeleo. Ndugu Makame amefafanua kuwa ili kupunguza msongamano na foleni za wagonjwa hospitalini, ni lazima jamii ianzie na usafi wa mazingira majumbani mwao kwani kuweka mazingira safi ndio njia kuu ya kujikinga na kuzuia milipuko ya maradhi mbalimbali.

Sauti ya Mwenyekiti wa Baraza la Mji Kusini, Ndugu Makame Ramadhan Makame