Mtegani FM

Polisi Zanzibar waja na operesheni ya kofia ngumu

16 October 2026, 11:23 am

Picha ikionesha Polisi na dereva wa boda boda wakishikilia mabango ya uzinduzi wa kampeni ya uvaaji wa kofia ngumu kwa waendeshaji wa vyombo vya maringi mawili Zanzibar, picha na Miraji Manzi Kae.

Jeshi la Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi limeendelea na operesheni kali ya kukamata madereva wa vyombo vya moto na abiria wanaokiuka sheria za usalama barabarani, huku likisisitiza kuwa uvaaji wa kofia ngumu (helmet) ni takwa la kisheria na sio hiyari.

Na Miraji Manzi Kae

Akitoa taarifa ya muendelezo wa operesheni hiyo, Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani Wilaya ya Mjini, Mrakibu Msaidizi wa Polisi (ASP) Abdulhakim Makame, ameeleza kuwa operesheni hiyo imeonyesha mwitikio mkubwa na wa kuridhisha kutoka kwa wananchi.

ASP Abdulhakim amebainisha kuwa katika siku ya kwanza ya operesheni hiyo, jumla ya pikipiki 103 zilikamatwa kwa makosa mbalimbali ikiwemo kutovaa kofia ngumu, kutokuwa na leseni halali za udereva, na vyombo kutokidhi viwango vya usalama. Hata hivyo, katika siku ya pili ya operesheni hiyo , idadi ya pikipiki zilizokamatwa ilipungua hadi 23, jambo linaloonyesha kuongezeka kwa uelewa na utii wa sheria kwa wananchi.

Operesheni hii ni sehemu ya utekelezaji wa Kampeni ya kuhamasisha uvaaji wa kofia ngumu Mkoa wa Mjini Magharibi, iliyoratibiwa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi, ACP Elthon Paul Banzi, na kuzinduliwa rasmi tarehe 3 Oktoba 2026 na Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi, Mhe. Mohd Ali Abdallah.

Kampeni hiyo inaendeshwa chini ya kaulimbiu isemayo: “Tii sheria bila shuruti, Vaa helmet, Ubongo hauna spea.” Lengo kuu ni kupunguza vifo na majeraha makubwa yanayotokana na ajali za barabarani, hasa kwa watumiaji wa vyombo vya usafiri wa miguu miwili.

Sauti ya Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani Wilaya ya Mjini, Mratibu Msaidizi wa Polisi (ASP) Abdulhakim Makame

Akiungana na wito wa Jeshi la Polisi, Dismas Philipo, dereva wa pikipiki (bodaboda) kutoka kituo cha Kisauni Wilaya ya Magharibi B, amewataka madereva wenzake na abiria kujenga tabia ya kuvaa kofia ngumu ili kujikinga na madhara makubwa pindi ajali zinapotokea. Dismas ameahidi kuendelea kutii sheria za usalama barabarani kwa usalama wake mwenyewe na wa abiria wake

Picha ikionesha baadhi ya ya boda boda wakipewa elimu ya uvaaji kofia ngu wakiwa kijiweni kwao kwa kazi ,Picha na Miraji Manzi Kae

Jeshi la Polisi limesisitiza kuwa operesheni hiyo ni endelevu na hatua kali za kisheria zitaendelea kuchukuliwa dhidi ya madereva au abiria wote wanaokiuka sheria bila ushuruti.