Mtegani FM

Watu 9 mbaroni kwa tuhuma za mauaji ya mtoto Raiyan, Pemba

22 October 2026, 11:52 am

Picha kutoka Mtandaoni

Jeshi la Polisi Mkoa wa Kaskazini Pemba linawashikilia watu tisa kwa tuhuma za kuhusika na mauaji ya mwanafunzi Raiyan Hemed Amour, mwenye umri wa mwaka 15, aliyepatikana amefariki dunia katika Kijiji cha Kwale Mpona, Shehia ya Finya, Wilaya ya Wete

Na Miraji Manzi Kae

Akitoa taarifa hiyo kwa waandishi wa habari, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kaskazini Pemba, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) William Mwampaghale, amesema Raiyan aliripotiwa kupotea Oktoba 2, 2026, kabla ya mwili wake kugundulika Oktoba 4, 2026, majira ya saa 3:20 asubuhi ukiwa katika kichaka kijijini hapo

Kamanda Mwampaghale ameeleza kuwa wakati mwili wa mwanafunzi huyo ukipatikana, ulikuwa na majeraha yakionyesha kukatwa kiganja cha mkono wa kulia kwa kutumia kitu chenye ncha kali

Anakamatwa kwa watuhumiwa hao tisa ni sehemu ya operesheni na msako mkali unaoendeshwa na jeshi hilo. Katika kipindi cha kuanzia Septemba 23 hadi Oktoba 21, 2026, Jeshi la Polisi limewakamata zaidi ya watu 20 wanaotuhumiwa kwa makosa mbalimbali ya jinai ikiwemo mauaji na wizi

“Upelelezi wa kina kuhusiana na tukio hili unaendelea, na mara utakapokamilika, watuhumiwa wote watafikishwa mahakamani ili hatua stahiki za kisheria zichukuliwe dhidi yao,” amesisitiza Kamanda Mwampaghale

Sauti Ya Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kaskazini Pemba, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) William Mwampaghale

Zaidi ya hayo, Jeshi la Polisi limetoa wito kwa wananchi kuendelea kufuata sheria na kushirikiana kwa karibu na vyombo vya ulinzi na usalama ili kudumisha amani na utulivu katika Mkoa huo na nchi kwa ujumla.