Mtegani FM

Binti wa miaka 19 ajinyonga baada ya kushinikizwa kutoa ujauzito

28 September 2026, 12:02 pm

Picha kutoka mtandaoni ikionesha kitanzi

Simanzi na majonzi vimetanda katika Kijiji cha Pete, Wilaya ya Kusini Unguja, baada ya msichana mmoja aliyetambuliwa kwa jina la Azmina Ismail Pandu (19), kupatikana amefariki dunia kwa kujinyonga juu ya mti.

Na Miraji Manzi Kae

Mwili wa marehemu ulipatikana majira ya asubuhi katika maeneo ya Pete, ukiwa unaning’inia kwenye mti wa mkeshia huku akiwa ametumia mtandio wake kujitoa uhai

Uchunguzi wa awali na taarifa za ufuatiliaji zinaonyesha kuwa chanzo cha msiba huo kinahusishwa na msukumo wa kisaikolojia na shinikizo alilolipata baada ya kugundulika kuwa ni mjamzito, huku akiwa hana mtu wa kumpa ushauri au mwongozo sahihi katika kipindi hicho kigumu. Ujumbe mfupi wa maandishi (SMS) uliopatikana kwenye simu ya mkononi ya marehemu ulionyesha mawasiliano kati yake na mwanamume mmoja aliyekuwa akimshinikiza aitoe mimba hiyo. Katika majibizano hayo, Marehemu Azmina alionekana kukataa kwa dhati wazo la kutoa mimba na badala yake alimtishia mwanamume huyo kuwa ataenda kujinyonga, vitisho ambavyo kwa bahati mbaya alivitekeleza

Sauti ya shuhuda akielezea namna tukio lilivyotokea Pete

Kabla ya kugundulika kwa mwili wake, familia na ndugu wa marehemu walikuwa katika juhudi kubwa za kumtafuta bila mafanikio baada ya kutojua alipo. Baada ya kutoa taarifa za kupotea kwake katika kituo cha polisi, siku iliyofuata ndipo walipopokea taarifa za kusikitisha za kuonekana kwa mwili huo

Tukio hili limeacha simanzi kubwa kwa wanafamilia na jamii nzima ya Pete, huku likiibua tena mjadala kuhusu athari za shinikizo la kutoa mimba na ukosefu wa msaada wa kisaikolojia kwa mabinti wadogo.