Mtegani FM

Vijana 40 kusini unguja waozeshwa kwenye mfumo wa aina yake Zanzibar

21 September 2026, 2:24 pm

Picha ikionesha baaddhi ya watu waliohudhuria katika harusi katika msikiti mkuu wa paje, picha na miraji manzi kae.

Jumla ya vijana 40 kutoka Mkoa wa Kusini Unguja, Zanzibar, wamefanikiwa kuingia kwenye maisha ya ndoa kwa pamoja, katika hafla ya kipekee iliyofanyika kwenye Msikiti Mkuu wa Paje.

Na Miraji Manzi Kae

Ndoa hizo zimesimamiwa kwa pamoja na Masheikh kutoka Ofisi ya Mufti wa Zanzibar ikishirikiana na Ofisi ya Wilaya ya Kusini Unguja, ambapo zoezi hilo limetajwa kuwa la kwanza la aina yake kufanyika visiwani humo kwa utaratibu wa kusaidia mahari.

Kwa mujibu wa waandaaji, miongoni mwa vigezo vikuu vilivyotumika kuwapata wanufaika hao ni pamoja na kijana kuwa na shughuli halali ya kujipatia kipato, mahali pa kuishi, na uwezo wa kuhudumia familia kwa mujibu wa miongozo na matakwa ya Dini ya Kiislamu. Mbali na kutoa mahari, mfadhili kutoka nje ya nchi aliyefanikisha mpango huo pia aligharamia mavazi ya maharusi, chakula cha mchana pamoja na usafiri kwa wahusika wote.

Picha ikionesha baadhi ya mabwana harusi ambao wamefunga ndoa katika msikiti mkuu wa paje, picha na miraji manzi kae

Wakizungumza mara baada ya kufungishwa ndoa hizo, baadhi ya mabwana harusi walieleza kuwa walikuwa na uwezo wa kuhudumia familia kupitia shughuli zao za kila siku, lakini changamoto kubwa ilikuwa ni kukusanya kiwango kikubwa cha mahari kinachowekwa na wazazi kwa wakati mmoja. Waliongeza kuwa kupokea msaada wa aina hiyo si jambo la aibu, bali ni fursa iliyowasaidia kutimiza sunna na kuondokana na vishawishi.

Sauti Ya Mkuu Wa Wilaya Ya Kusini Unguja