Mtegani FM

Tamwa-Zanzibar yaitaka polisi kuharakisha uchunguzi mauaji ya Raiyan Pemba

7 October 2026, 12:35 pm

Picha ikimuonesha Mkurugenzi wa Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania, Zanzibar (Tamwa-ZNZ)  Bi. Nairat Abdulla Ali Akizungumza na waandishi wa habari, picha na Miraji Manzi Kae.

Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania, Zanzibar (TAMWA-ZNZ) kimeomba Jeshi la Polisi kuharakisha uchunguzi wa kina kuhusu kifo cha mtoto Raiyan Hemed Amour (15), mwanafunzi wa kidato cha kwanza katika Skuli ya Sekondari Kizimbani, Wilaya ya Wete, Mkoa wa Kaskazini Pemba.

Na Miraji Manzi Kae

Kulingana na taarifa iliyotolewa na Jeshi la Polisi mnamo Oktoba 5, 2026, mwili wa Raiyan uligunduliwa katika kichaka akiwa amefariki dunia baada ya kutoweka nyumbani kwao Kijiji cha Kwale Mpona tangu Ijumaa, Oktoba 2, 2026, alipokuwa akielekea skuli. Mwili wake unadaiwa kukutwa katika kichaka huku kiganja chake cha mkono wa kulia kikionekana kukatwa kwa kitu chenye ncha kali.

TAMWA-ZNZ imesisitiza kuwa uchunguzi wa kina na wa haraka unahitajika ili kuwatafuta na kuwachukulia hatua kali za kisheria waliohusika na kitendo hicho cha ukatili. Hatua hiyo imetajwa kuwa muhimu katika kujenga imani ya wananchi kwa mifumo ya haki na kutoa ujumbe mzito kwamba jamii haitavumilia vitendo vya ukatili dhidi ya watoto

Pia, shirika hilo limeitaka Serikali na mamlaka husika kuimarisha usalama wa mazingira wanayopitia watoto wanapokwenda na kurudi skuli, ikiwa ni pamoja na kusafisha au kuondoa vichaka na maeneo hatarishi yaliyo karibu na makazi pamoja na njia zinazotumiwa na wanafunzi

TAMWA-ZNZ imekumbusha kuwa tangu mwishoni mwa mwaka 2016, imeshuhudia jumla ya matukio 34 ya mauaji ya wanawake (27) na watoto (7). Hata hivyo, imeelezwa kuwa jamii haijaripotiwa kikamilifu kuhusu mwenendo na hukumu za kesi hizo, jambo linalohitaji kubadilika ili kuongeza uwazi, uwajibikaji, na imani katika mifumo ya haki

Zaidi ya hayo, TAMWA-ZNZ imeiomba Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali ikishirikiana na Wizara ya Afya kutoa huduma za msaada wa kisaikolojia (psycho-social support) kwa watoto na wanafunzi wa Kijiji cha Kwale na maeneo ya jirani ili kuwasaidia kukabiliana na hofu, msongo wa mawazo, na mshtuko uliotokana na tukio hilo la kusikitisha

Tukio hili linagusa utekelezaji wa Malengo Endelevu ya Maendeleo (SDGs), hasa Lengo la 5 (Usawa wa Jinsia na Kukomesha Ukatili) na Lengo la 16 (Amani, Haki na Taasisi Imara)

TAMWA-ZNZ imetoa pole za dhati kwa familia, ndugu, walimu, na wanafunzi wenzake na marehemu Raiyan Hemed Amour katika kipindi hiki kigumu.