Micheweni FM

Serikali ya Zanzibar Kuimarisha Elimu ya Ufundi na Uhandisi

18 February 2026, 2:13 pm

Waziri wa elimu na mafunzo ya amali Zanzibar Mh Leila Mohd Mussa akizungumza na wananchi pamoja na wakandarasi wa ujenzi wa skuli ya ufundi (picha Ali Kombo)

Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imesema itaendelea kuwekeza katika elimu ya ufundi na uhandisi ili kuzalisha wahandisi wazawa watakaosimamia miradi ya maendeleo nchini.

Na Ali Kombo

Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali, Lela Muhamed Mussa, amesema hayo wakati akikabidhi eneo la ujenzi wa Skuli ya Ufundi Mikunguni wilaya ya Mjini Unguja, ikiwa ni sehemu ya shamrashamra za siku 100 za uongozi wa Rais Dk. Hussein Ali Mwinyi.

Ujenzi wa skuli hiyo utagharimu shilingi bilioni 8.6, na utahusisha madarasa 16, maabara za kisayansi na kompyuta, pamoja na warshtati za ufundi seremala na umeme wa jua.

Waziri amewataka wazazi kushirikiana na watoto wao waliopata nafasi ya kusoma fani ya uhandisi na kutozibadilisha wanapofika vyuo vikuu, kwani serikali imeondoa ada kwa wanafunzi wa ufundi.

Mkandarasi wa mradi huo Fakih Abdalla Pandu, ameahidi kukamilisha ujenzi kwa muda uliopangwa, ili wanafunzi wapate kutumia majengo mapya kuanzia mwaka ujao.

Mwalimu Mkuu skuli ya Ufundi Mikunguni, Tifli Mustafa Nahoda, alisema skuli hiyo ina wanafunzi 250 ambayo ilikua na madarasa 9, vyoo 18 na ufaulu wao ulikua mzuri hivyo wanatarajia kutoa wataalamu wabobezi watakapopata jengo la kisasa.