PEGAO yataja mwarubaini wanawake kushika hatamu
6 October 2021, 11:34 am
Na Zuhura Juma.
WANANCHI wametakiwa kushirikiana pamoja katika kuwainua wanawake, ili kuhakikisha wanakuwa viongozi kuanzia ngazi ya jamii hadi Taifa.
Akizungumza na wananchi wa shehia ya Tumbe Magharibi, Mkurugenzi wa Jumuiya ya PEGAO Pemba Hafidh Abdi Said amesema, wanawake wanao uwezo wa kuongoza na kuleta mabadiliko ya haraka, hivyo ni vyema jamii ikampa mashirikiano katika kuusaka uongozi.
Amesema, katika jamii kuna vikundi na Jumuiya mbali mbali zinazoanzishwa kwa ajili ya kuleta maendeleo, ingawa kinachomshangaza ni kuona kuwa wanawake hunyimwa hata nafasi hizo, jambo ambalo sio sahihi kwani wanawafanya waendelee kubaki nyuma kila siku zinaposonga mbele.
Aidha amewataka akinababa kuwaunga mkono akinamama wanaotia nia ya kugombea uongozi, kwani kila mmoja anamtegemea mwenzake katika harakati mbali mbali za kijamii, kisiasa na kiuchumi katika kufikia malengo.
Akiwasilisha mada katika mkutano huo Mudathir Sharif Khamis amesema, kuwa kila mmoja yuko sawa mbele ya Sheria, hivyo si vyema kumnyima mwanamke kugombea uongozi kwa kisingizio cha kuwa yeye ni mama wa nyumbani.
Nae muwasilishaji Hadia Sultan Hamad ameeleza, kuna baadhi ya wanajamii humkwamisha mwanamke katika kugombea nafasi hizo kwa kisingizio cha dini, jambo ambalo so sahihi kwani zamani walikuwepo wanawake wa kiislamu ambao walikuwa wakisimamia mambo mbali mbali katika jamii zao.
Kwa upande wake Maryam Hemed Said mkaazi wa Tumbe ameeleza kuwa, wanawake ambao ni viongozi wameleta mchango mkubwa katika jamii na juhudi mbali mbali zinaonekana katika kuliletea Taifa maendeleo.
Akichangia katika mkutano huo Ali Mohamed Bakar amesema kuwa, wanawake wanashindwa kufikia uongozi kutokana na mifumo ya kiutawala iliyopo katika vyama, kwani huwekewa vizingiti vikubwa.
Kwa upande wao wananchi wengine walisema kuwa, kumekuwa na viongozi kwenye majimbo ambao huwashawishi wapiga kura wasimpe mwanamke na kuwabandikiza chuki zisizo na sababu, jambo ambalo linawaumiza sana wanaogombea.