TAMWA ZNZ yasaidia utatuzi wa uharibifu wa Mazao ya Wajasiriamali Pemba
5 October 2021, 2:34 pm
CHAMA cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania, Zanzibar- TAMWA-ZNZ leo octoba 05,2021 kimekabidhi Waya wa uzio kwaajili ya kuweka kwenye shamba la wajasiriamali linalomilikiwa na kikundi cha TUSIFE MOYO kilichopo Shehia ya Kangagani, Wilaya ya Wete mkoa wa Kaskazini Pemba ili kudhibiti uharibufu wa mazao unaofanywa na wanyama katika shamba hilo.
Akikabidhi waya huo, mratibu wa TAMWA ofisi ya Pemba, Fat-hiya Mussa amesema kutolewa kwa waya huo kumekuja kufuatia wajasiriamali hao waliowezeshwa na TAMWA-ZNZ kupitia mradi wa kuwawezesha wanawake kiuchumi Zanzibar, (WEZA III) kukabiliwa na tatizo la uharibifu wa mazao unaofanywa na wanyama wa kufugwa jambo linalopelekea kushindwa kuzalisha ipasavyo.
Amesema baada ya ziara ya meneja miradi wa TAMWA-ZNZ, Ali Mohammed aliyoifanya Agosti 27 mwaka huu kugundua uwepo wa changamoto hiyo katika kikundi hicho, TAMWA ZNZ kimechukua juhudi za kuhakikisha inasaidia utatuzi wa tatizo hilo ili wajasiriamali waendelee na uzalishaji kwaajili ya kufanikisha lengo la mradi kuwainua wanawake kiuchumi kupitia shughuli zao.
Licha ya wajasiriamali hao kuwezeshwa waya huo lakini pia amewataka kuimarisha ulinzi wa mazao yao ili kudhibiti uharibifu unaofanywa shambani ikiwa ni pamoja na wizi wa mazao.
Mwenyekiti wa kikundi hicho, Fatma Ali Msanifu ameishukuru TANWA ZNZ kwa kusaidia waya huo kwani utasaidia kukomesha uharubifu huo jambo ambalo lilikuwa linawakatisha tamaa kuendelea na uzalishaji.
Mradi wa Kuwawezesha wanawake kiuchumi Zanzibar (WEZA III) unatekelezwa na TAMWA-ZNZ kwa kushirikiana na Milele Zanzibar Foundation.