MWENYEKITI wa Baraza la Vijana wilaya ya kati afanya ziara Wilaya ya Micheweni
4 October 2021, 10:33 am
Na Said Abdalla: MWENYEKITI wa Baraza la Vijana Wilaya ya kati Unguja Omar Khamis Omar amefanya ziara katika wilaya ya Micheweni mkoa wa Kaskazini Pemba kwa ajili ya kubadilishana mawazo na kutembelea miradi mbalimbali ya wilaya hiyo.
Wakati wa ziara hiyo Omar Khamis amesema amevutika na mambo mbalimbali yanayofanywa na baraza la vijana wilaya ya micheweni kwani ni mambo yanayoleta motisha na kufungua milango ya umoja kwa wana jamii.
Mbali na hayo mwenyekiti huyo amewapongeza viongozi mbalimbali wa chama na Serikali kwa kuwaunga mkono vijana jambo ambalo limekuwa adimu kwao.
Aidha amemtaja mkuu wa wilaya ya Micheweni Mgeni Khatib Yahya kuwa mfano bora kwa viongozi kwani mchango wake kwa vijana unaonekana na kusema kuwa endapo mashirikiano hayo atayaendeleza basi baada ya miaka mitatu Micheweni itakuwa wilaya ya mfano kwa Zanzibar.
Kwa upande wake katibu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) wilaya ya micheweni Hasaan Khatib Hassan amemshukuru mwenyekiti huyo kwa ujio wake na kuahidi kuwa kama viongozi wa chama wilaya wataendelea kushirikiana na wilaya ya kati unguja ili kupanua fursa mbalimbali za mabaraza ya vijana
Katika hatua nyengine Katibu wa CCM amewapongeza wanabaraza wilaya ya Micheweni kwa kutekeleza ilani ya CCM kwa vitendo kwani Serikali kupitia rais wa Zanzibar na mwenyekiti wa baraza la Mapinduzi dkt Hussein Ali Mwinyi inajitahidi sana kuweka misingi na vipaumbele vya kuwasaidia vijana wa Zanzibar.
Nae katibu wa idara ya siasa, itikadi na uenezi wilaya ya micheweni Abdalla Khamis Shaame amewapongeza viongozi wa wilaya ya kati kwa kufanya ziara katika wilaya hiyo kwani ni moja kati ya nyezo muhimu ya urafiki na utekelezaji wa azma na matakwa ya Serikali.
Mapema akisoma risala fupi Mwenyekiti wa baraza la vijana wilaya ya Micheweni Is-haka Khamis Shaame amesema katika wilaya ya Micheweni kuna darasa la ufundishaji wa lugha za kigeni ambalo limeanzishwa kwa lengo la kuwainua vijana kiuchumi kupitia fursa mbalimbali za kiuwekezaji amabazo zinaendelea kufanywa katika wilaya hiyo.
Amesema darasa la lugha limeanzishwa baada ya kikao muhimu cha kamati ya uchumi wa buluu kukaa pamoja na Jumuiya ya watu wa uhifadhi wa urithi Pemba kuweza kuomba kuanzishwa darasa hilo.
Baraza la Vijana Wilaya ya Micheweni hadi sasa wana miradi mbalimbali iliyojumuisha Kilimo, Biashara, Uzalishaji, Ufundi pamoja na vikundi vya Sanaa.