Wakulima 50 Pemba wanufaika na vifaa kupitia mradi wa VIUNGO
1 October 2021, 9:17 am
Na Gaspary Charles
JUMLA ya wakulima hamsini wa bustani za nyumbani Kisiwani Pemba katika kipindi cha mwaka wa kwanza wa utekelezaji mradi wa Viungo, Mboga na Matunda wamewezeshwa vifaa vya kilimo ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa mradi huo unaolenga kufungua fursa na kuongeza mnyororo wa thamani kwa mazao hayo visiwani Zanzibar.
Utolewaji wa vifaa hivyo kwa wakulima hao umekuja baada ya wakulima kupata fursa ya kujifunza mbinu za uzalishaji na uendeshaji wa bustani hizo kupitia mfumo wa shamba darasa zilizoanzishwa katika maeneo mbalimbali ambayo mradi unatekelezwa.
Rehema Abdrahman Alawi ambaye ni afisa wa mradi huo alisema utoaji wa vifaa hivyo umekuja kwa lengo la kuwawezesha wakulima kuwa na nyenzo muhimu za kutumia taaluma waliyojifunza kutoka kenye shamba darasa na kwenda kuzitumia katika maeneo yao.
“Lengo la mradi kutoa vifaa hivi ni kuhakikisha wakulima wanapata kuutumia vizuri ujuzi wa matumizi ya teknolojia mbalimbali waliyojifunza katika shamba darasa kwenye uendeshaji wa bustani hizo majumbani mwao,”
Rehema
Aliongeza kuwa mradi huo utaendelea kuwezesha vifaa hivyo kwa wakulima katika kila hatua ili kuhakikisha malengo ya mradi yanafikiwa kwa wakati katika kipindi cha utekelezaji wa mradi huo.
Katika hatua nyingine aliwasisitiza wakulima walionufaika na vifaa hivyo kufuata maelekezo ya matumizi yake ili viweze kuleta tija kwenye shughuli zao za kilimo.
Aidha aliwataka wananchi wa maeneo ambayo mradi unatekelezwa kujitokeza kujifunza taaluma mbalimbali kupitia kwa wakulima hao ili nao wakaendeleze katika maeneo yao kutokana na mradi kuhitaji kuwafikia wakulima wengi zaidi kupitia wakulima viongozi.
“Wananchi wa maeneo ambayo mradi unatekelezwa waendelee kujitokeza kujifunza kupitia kwa wakulima hawa ambao tumewawezesha vifaa hivi ili nao wakaendeleze taaluma hii katika maeneo yao kwani hilo ndilo lengo la mradi huu kuhakikisha kila mwananchi ananufaika kwa namna moja au nyingine.”
Rehema
Fatma Moh’d Abeid alisema vifaa hivyo vitasaidia kuongeza kasi ya uzalishaji wa mboga kupitia bustani za nyumbani kutokana na kikwazo chao kikubwa ilikuwa ni ukosefu wa nyenzo za kisasa katika kuendeshea bustani hizo.
Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania, Zanzibar, (TAMWA ZNZ), People’s Development Forum (PDF) na Community Forests Pemba (CFP) ni watekelezaji wa mradi huo wa miaka minne wenye lengo la kufungua fursa za masoko na kuongeza mnyororo wa thamani kwa mazao hayo Zanzibar kupitia ufadhili wa Umoja wa Ulaya (EU)