SMZ yaainisha mikakati kutekeleza kwa vitendo dhana ya uchumi wa buluu
28 September 2021, 6:36 pm
NA MWIABA KOMBO.
SERIKALI ya Mapinduzi Zanzibar imejipanga kikamilifu kuhakikisha wanafanikiwa katika dhana ya uchumi wa buluu katika kuhamasisha matumizi zaidi na endelevu ya bahari kwa ajili ya upatikanaji wa ajira za kudumu.
Akizungumza katika mkutano wa wadau kuhusu mapitio ya rasimu ya uchumi wa buluu katika Ukumbi wa Kiwanda cha Makonyo Chake Chake Mkuu wa Mkoa wa Kusini Pemba Matar Zahor Massoud amesema, maamuzi hayo ya uwekezaji wa uchumi wa bahari yamefikiwa kwa kutambua uwezo na mpango wa maliasili na rasilimali za pwani na baharini zinazozunguka visiwa vya Zanzibar.
Amesema kuwa, sekta ya uvuvi ni muhimu kwa maendeleo ya Zanzibar, hivyo Serikali inafanya jitihada za dhati za kuendeleza uvuvi wa bahari kuu, ili kuzalisha ajira kwa wananchi na kuweza kijipatia kipato kitakachowasaidia kuwakwamua na maisha duni.
Aidha amesema kuwa, Serikali ya awamu ya nane imejikita katika kuboresha masoko ya samaki yaliyopo na kujenga mapya, ambapo suala hilo litakwenda sambamba na ujenzi wa Kiwanda cha kuchakaza minofu na kusindika samaki kwa ajili ya kuuza ndani na nje ya Zanzibar.
Akitaja vipaoumbele ni sekta ya uvuvi mdogo mdogo na wa bahari kuu, ufugaji wa samaki, uchimbaji wa mafuta na gesi, pamoja na utalii wa fukwe na michezo ya baharini.
Akiwasilisha mada ya dhana ya uchumi wa buluu Afisa Uratibu Shaaban Hassan Ramadhan amesema kuwa, ni matumizi endelevu ya rasilimali za baharini, mito na maziwa kwa ajili ya ukuzaji uchumi, maendeleo ya kijamii na uhifadhi wa mazingira.
Nae Mjumbe wa Timu ya Maandalizi ya Sera ya Uchumi wa Buluu Kitwana Makame Kitwana amesema, Serikali itahakikisha inaimarisha usafiri wa bandarini sambamba na uendeshaji wa viwanda unaokidhi haja.
Mapema Afisa Mdhamini Wizara ya Uchumi wa Buluu na Uvuvi dk Salim Mohamed Hamza amesema amewataka viongozi hao kuwa na sauti ya pamoja katika kuwaelezea wananchi juu ya Sera ya Uchumi wa Buluu ili waweze kuifahamu na kuifanyia kazi hasa kwa wale wanaojishugulisha na kazi za baharini.
Akichangia mada katika mkutano huo Afisa Mdhamini Tume ya Mipango Pemba Khamis Issa Mohamed ameeleza kuwa, wananchi wa Zanzibar bado hawajaelewa dhana ya uchumi wa buluu, hivyo juhudi za makusudi zinahitajika kuwaelimisha.
Mkutano huo wa siku mbili kwa wadau mbali mbali ulifanyika katika Ukumbi wa Kiwanda cha Makonyo, ambapo mada mbali mbali ziliwasilishwa ikiwemo sera ya uchumi wa buluu, mpango wa wavuvi na dhana ya uchumi wa buluu.