Olengurumwa apongeza kikao cha Rais Samia, wananchi Ngorongoro
2 December 2024, 1:25 pm
Katika kuhakikisha changamoto zinazowakabili wananchi wa Ngorongoro zinatatuliwa Rais Samia akutana na viongozi wa serikali pamoja na wale wa kimila wanaoishi Ngorongongoro ili kuona namna bora ya kutatua changamoto hizo.
Na Saitoti Saringe
Akizungumza Desemba Mosi 2024 Olengurumwa amesema anapongeza hatua ya Mh Rais Samia kukutana na wananchi wa Ngorongoro hasa wa tarafa ya Ngorongoro pamoja na Loliondo kutokana na changamoto zinazowakabili wananchi hao baada ya muda mrefu wananchi hao kutaka kuonana na Rais Samia.
Aidha wakili Olengurumwa amesema wao kama mtandao wa watetezi wa haki za binadamu Tanzania mara nyingi wamekuwa wakipendekeza Mhe Rais kukutana na wananchi wa Ngorongoro ili kusikiliza changamoto zao hivyo ni faraja kwao kuona kwamba Rais amekutana na wananchi hao baada ya kuwatuma mawaziri katika zile hatua za awali katika sakata la Ngorongoro na kuona utekelezaji wa yale maagizo ya urejeshwaji wa huduma za kijamii katika tarafa ya Ngorongoro.
Katika hatua nyingine Olengurumwa ameongeza kuwa kitendo cha Rais kukutana na wananchi hao inaongeza nguvu ya kutatua changamoto zaidi katika eneo hilo la Ngorongoro.
Hata hivyo Olengurumwa ameshauri iundwe tume huru ya kuchunguza sakata hilo na kuweza kumshauri Rais katika njia bora ya kutatua tatizo la Ngorongoro kama ambavyo wamekuwa wakiandika katika taarifa zao kama Watetezi wa haki za binadamu kwani wamekuwa wakisisitiza umuhimu wa kuwa na Tume huru kwa ajili ya kutatua Suala la Ngorongoro huku akisema kuwa tume hiyo itakayoundwa iwe shirikishi kwa wananchi ili tume hiyo iweze kuzingatia ushirikishwaji wa wananchi, makundi yote yaliyokuwa wanafuatilia suala hilo ili kusaidia serikali kutatua changamoto za Ngorongoro na hatua za kuhifadhi maeneo yale yaendane na misingi ya haki za binadamu na si kulinda tu maeneo yale bali kustawisha maisha ya wananchi wa eneo hilo.
Kikao hicho kilichofanyika ikulu ndogo jijini Arusha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. Samia Suluhu Hassan ameahidi kuwa ataunda tume mbili ambapo moja itachunguza na kutoa mapendekezo kuhusu masuala ya ardhi yanayolalamikiwa na wakazi wa Ngorongoro, Tume nyingine itaaangalia utekelezaji wa zoezi zima la uhamiaji kwa hiari kutoka eneo la Hifadhi ya Ngorongoro.
Kikao hicho kimeudhuriwa na Viongozi wa serikali, Viongozi wa kimila (Malaigwanani) na baadhi ya wananchi wanaoishi tarafa ya Ngorongoro na Loliondo.