Loliondo FM

Mchengerwa: Marufuku wananchi kuhamishwa kwenye maeneo ya malisho

6 October 2024, 5:38 am

Waziri wa nchi,ofisi ya rais tawala za mikoa na serikali za mitaa (TAMISEMI) mh Mohamed (Picha na mpiga picha)

Kumekuwepo na viongozi wa mikoa au wilaya kutoa maelekezo ya kuwahamisha wafugaji katika maeneo yao ambayo ni malisho ya mifugo yao kwa kisingizio cha kufuata maelekezo ya mh rais.

Na mwandishi wetu .

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mh. Mohamed Mchengerwa amewaonya baadhi ya viongozi wa serikali wanaowashawishi na kutaka kuwaondoa wananchi wanaoishi maeneo ya malisho ambayo serikali ilisharidhia na kutoa tangazo la serikali (GN) kuruhusu wananchi hao kuendelea kuishi maeneo hayo.

Amesema amesikia kwenye baadhi ya maeneo mkoa wa Arusha kuna mchakato wa kuwaondoa wananchi kwenye maeneo hayo huku wengine wakiwashawishi na kutumia sauti ya rais kwamba anawataka waondoke kwenye maeneo hayo wakati siyo kweli.

Mh. Mchengerwa ametoa maagizo hayo Oktoba 06, 2024 katika ziara yake Halmashauri ya Jiji la Arusha na kuzitaja wilaya za Arumeru, Monduli,Karatu,Longido na Ngorongoro kuwa kuna baadhi yao wamekuwa wakiwashawishi na kutaka kuwaondoa wananchi katika maeneo hayo wakidai yanapimwa kwa ajili ya matumizi mengine.

Kutokana na hilo amemwagiza Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mh. Paul Makonda kusimamia wilaya hizo na kuwa serikali ilishatangaza tangazo la serikali na maeneo hayo mchakato wa uchaguzi unaendelea ikiwemo kujiandikisha.

Amesema serikali haitasita kumchukulia hatua kiongozi yoyote atakayehusika na mchakato wa kuwaondoka wananchi wanaoishi katika maeneo ya malisho.

Ameongeza kuwa wakuu wa wilaya za Arumeru, Monduli, Karatu, Longido na Ngorongoro kuwepo kwa changamoto ya suala la malisho na wapo wananchi ambao wametakiwa kuhama kwenye maeneo yao hivyo maelekezo yake ndiyo maelekezo ya rais na tangazo la serikali linapotolewa hiyo ndiyo mipaka halali ya wananchi.

Hata hivyo mh Mchengerwa amesema hakuna mtu mwingine mwenye mamlaka ya kuwaondoa wananchi mpaka pale mipaka hiyo itakaporekebishwa na waziri wa tamisemi na maeneo hayo wameridhia wananchi wapige kura huku akikumbushia tangazo la serikali kusomwa Arusha.

Amehitimisha kuhusu kuwepo kwa michakato ya kuwaondoa wananchi kwenye maeneo ya malisho kuendelea na taratibu za kuwaondoa,kuwashawishi na viongozi wengine wakitumia sauti ya rais kwamba ametaka waondoke, akidai kuwa ni kumchongisha rais na wananchi huku akiwaonya wakuu wa wilaya asisikie kiongozi yoyote wa serikali za mitaa akiwaondoa wananchi.