Loliondo FM

Ashambuliwa na sime kisa kulisha ng’ombe chumvi Ngorongoro

12 June 2024, 7:14 pm

Kijana Mutari Yaile akiwa Hospitali teule ya Wasso akipatiwa matibabu baada ya kushambuliwa na kundi la vijana(picha na Edward Shao).

Mkuu wa mkoa wa Arusha Mh Paul Makonda wakati anawasili kwa mara ya kwanza mkoani hapa alinukuliwa akisema mkoa wa Arusha una migogoro mingi ya aridhi na kumpa kamishina wa Aridhi miezi mitatu kuhakikisha anaimaliza migogoro hiyo.

Na Edward Shao.

Kijana mmoja mkaazi wa kijiji cha Kirtalo Mutari Yaile (24) ameshambuliwa na kundi la vijana kisa kulisha ng’ombe katika eneo lenye mgogoro kati ya kijiji cha Kirtalo na Oloipir.

Tukio hili limetokea kati ya vijiji hivyo viwili Juni 11,2024 wakati kijana huyo akilisha ng’ombe chumvi eneo la Orikena lililopo tarafa ya Loliondo wilayani Ngorongoro.

Akizungumza akiwa anaendelea kupatiwa matibabu katika hospital teule ya Wasso majeruhi huyo bwn Mutari amesema,wakati akiwa analisha ng’ombe walijitokeza vijana watatu nakumuuliza kwanini anapitisha ng’ombe karibu na nyumbani na wakati akijibu walianza kumshambulia kwa sime na fimbo maeneo mbalimbali ya mwili wake.

Sauti ya Mutari

Kwa upande wake ndugu wa kijana huyo bwn John Tome amesema ndugu yao huyo alishambuliwa majira ya saa tisa alasiri wakati amekwenda kulisha ng’ombe chumvi ya asili eneo la Orikena na wakati akiendelea kuwalisha ng’ombe ndipo alipokumbwa na mkasa huo.

Sauti ya John Tome

Mganga mfawidhi wa hospitali teule ya Wasso Dr Filipina Adrian akizungumza na Loliondo fm amekiri kumpokea majeruhi majira ya saa 11:30 jioni akiwa na majeraha maeneo ya kichwani na kumpatia matibabu,ameongeza kuwa kwasasa wanakamilisha taratibu za kumpa rufaa kwenda hospitali kubwa kwa matibabu zaidi.

Sauti ya Dr Filipina Adrian

Mkuu wa wilaya ya Ngorongoro alipotafutwa kuzungumzia tukio hilo simu yake iliita bila mafanikio.

Mgogoro huu unaelezwa kudumu sasa kwa zaidi ya miaka 20 katika eneo hili ambalo awali liliwekwa kwenye mpango wa matumizi bora ya ardhi kupitia maazimio ya baraza la madiwani ili kuboresha nyanda za malisho kati ya kijiji cha Soit sambu na Oloipiri ambazo kwa sasa ni kata mbili tofauti.

Wananchi wa vijiji hivyo wanaomba viongozi wa mila, kisiasa na serikali kuingilia kati na kutafuta suluhu ya kudumu katika eneo hili, watu wengi hasa vijana wadogo wamepoteza maisha katika eneo hili na wengine kujeruhiwa mara kwa mara.