Loliondo FM
Loliondo FM
16 June 2025, 10:37 pm

Katika hatua ya kuimarisha mazingira ya gereza, Wakili Olengurumwa ambaye ni Mwenyekiti wa Ngorongoro Legal Aid Center ametoa vifaa vya ujenzi kwa ajili ya ukarabati wa bweni la wafungwa gereza la Loliondo.
Na Saitoti Saringe
Tukio hilo limefanyika tarehe 16.06.2025 katika gereza la Loliondo, Ngorongoro ambapo vifaa vya ujenzi vyenye thamani ya shilingi laki tisa vimekabidhiwa kwa viongozi wa gereza.
Akizungumza kwa niaba ya Wakili Ole Ngurumwa Mkurugenzi wa Ngorongoro Legal Aid Center mzee Ole Ndangoya amesema kuwa wao kama wadau wameamua kuisapoti Taasisi ya Magereza kwa kutambua umuhimu wa magereza katika jamii.
” Kwa niaba ya mwenyekiti wa NGOLAC wakili Olengurumwa tunakabidhi vifaa hivi vya ujenzi kama msaada wetu ambao unaweza kusaidia katika maendeleo ya gereza na tutaendelea kutoa mchango wetu kadri itakavyowezekana”
Kwa upande wake Mkuu wa gereza la Loliondo Mrakibu George Osindi ameishukuru Ngorongoro Legal Aid Center NGOLAC kupitia kwa mwenyekiti wake wakili Olengurumwa kwa kutambua jitihada za maendeleo yanayofanyika gerezani hapo kwa kutoa vifaa vya ujenzi vitakavyosaidia kuleta maendeleo katika gereza hilo.
Wakili Olengurumwa ambaye pia ni mratibu wa kitaifa wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania THRDC amekuwa akifika mara Kwa mara katika gereza hilo kutoa misaada mbalimbai.
Vifaa vilivyotolewa ni pamoja na mifuko 20 ya Saruji, Wire mesh 16 na Sinki za vyoo, ambapo vifaa hivyo vimegharimu jumla ya kiasi cha shilingi laki tisa.