Loliondo FM

Oloipiri yaongoza kuwa na watoto wenye hali mbaya ya lishe

25 May 2025, 10:34 am

Mkuu wa wilaya ya Ngorongoro Kanali Wilson Sakulo akiandika jambo katika kikao cha lishe, picha na Zacharia James).

Kata ya Oloipiri imetajwa kuwa miongoni mwa kata zenye hali mbaya ya lishe kwa watoto hali iliyopelekea mkuu wa wilaya ya Ngorongoro kutoa maagizo mazito kwa shule ambazo wanafunzi hawali chakula cha mchana shuleni.

Na Zacharia James.

Mkuu wa wilaya ya Ngorongoro Mhe. kanali Wilson Sakulo amewaagiza watendaji wa kata zote zenye shule zisizo na majiko ya kupikia chakula cha wanafunzi kujenga mara moja ili kutokomeza udumavu na kuboresha lishe kwa wanafunzi.

Ameyasema hayo Ijumaa ya Mei 23, 2025 katika kikao cha kamati ya lishe wilaya kilichoketi kutathimini hali ya lishe ya wilaya ya Ngorongoro katika kipindi cha robo ya tatu ya mwaka wa fedha 2024/25 Januari hadi Machi ambapo ametilia mkazo azimio la kikao cha kamati hio cha tarehe 19/12/2024 ambacho kiliazimia watendaji wa kata kuainisha shule zisizo na majiko na stoo za kuhifadhia chakua na kisha wawashirikishe wanachi kupitia vikao vya kata kuchangia ujenzi wa majiko na stoo hizo akisisitiza umuhimu wa upatikanaji wa chakula shuleni ni moja ya nguzo za utekelezaji wa viashiria vya lishe kitaifa.

Kwa upande wake afisa lishe wa halmashauri ya wilaya ya Ngorongoro Bi Angela Mbanga amesema hali ya utapiamlo imepungua kutoka asilimia 0.20 robo ya pili ya mwaka 2024/25 hadi asilimia 0.12 robo ya tatu ya Januari hadi Machi 2024/2025.

Amesema katika kipindi cha Januari hadi Machi 2025 upimaji unaonyesha jumla ya Watoto 44,795 kati ya watoto 64,084 wakiume 21,756 na wakike 23,039 sawa na asilimia 70 walifanyiwa taathmini ya hali ya lishe kwa kupimwa uwiano wa uzito kwa umri kupitia vituo vya kutolea huduma za afya na jumla ya watoto 43,244 wakiume 20,961 na wakike 22,283 sawa na asilimia97 walikua na hali nzuri ya lishe watoto 1,496 wakiume 770 wa kike 726 sawa na asilimia 3 waligundulika kuwa na hali hafifu ya lishe na Watoto 55 wakiume 25 na wakike 30 sawa na asilimia0.12 walikua na hali mbaya ya lishe.

Amefafanua kuwa maeneo yenye Watoto wenye hali mbaya ya lishe ni Kata za Oloipiri kati ya watoto 2,781 watoto 9 wana hali mbaya ya lishe,Sero kati ya watoto1,211 watoto 5 wana hali mbaya ya lishe,Olorien Magaiduru kati ya watoto 2,256 watoto 11 wana hali mbaya ya lishe na Orgosorok kati ya watoto1,220 watoto 10 wana hali mbaya ya lishe ikilinganishwa na robo iliyopita ambapo kata za Olbalbal kati ya watoto 531 watoto 5 walikuwa na hali mbaya ya Lishe, Kata ya Ngorongoro kijiji cha Oloirobi kati ya Watoto 572 watoto 9 walikuwa na hali mbaya ya Lishe na Kata ya Malambo kati ya watoto 1,836 watoto 12 walikuwa na hali mbaya ya lishe.

Sauti ya bi Angela Mbaga

Watoto waliobainika kuwa na hali mbaya ya lishe walifikishwa kwenye vituo vya kutolea huduma za afya hususani hospitali ya wilaya na hospitali ya Wasso kupatiwa matibabu stahiki ili kuboresha hali zao za lishe.