Loliondo FM
Loliondo FM
29 April 2025, 8:24 pm

Katika hatua ya kuimarisha maendeleo na huduma kwa jamii, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Ngorongoro, Mheshimiwa Mohammed Bayo amefanya ziara ya kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo katika eneo hilo. Ziara hiyo ililenga kutathmini maendeleo ya miradi inayotekelezwa na halmashauri pamoja na changamoto zinazokabiliwa na wananchi.
Na Saitoti Saringe
Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Ngorongoro Mhe Mohammed Bayo akiambatana na wataalamu kutoka halmashauri hiyo ametembelea miradi ya elimu, afya, na miundombinu ambapo alionesha kuridhishwa na maendeleo yaliyopatikana na kusisitiza umuhimu wa kushughulikia changamoto zinazojitokeza.
“Tuna dhamana ya kuhakikisha kwamba wananchi wetu wanapata huduma bora na zenye ubora. Ni lazima tuwekeze katika miradi hii ili kuboresha maisha ya watu wetu” alisema Mheshimiwa Bayo.
Katika ziara hiyo Mhe Bayo ametembelea pia shule ya msingi Olpiro na Zahanati ya Olpiro kata ya Eyasi ikiwa lengo nikujua hali ya maendeleo katika taasisi hizo na kujionea Hali ya uboreshaji uliofanyika kwani serikali ilitoa kiasi cha milioni 124 za awali za kufanyia maboresho ya miundombinu katika tarafa hiyo huku shule ya Olpiro ikitengewa kiasi Cha milioni sita kama kiasi cha awali.
Aidha, Mhe. Bayo ametumia nafasi hiyo kujibu changamoto ya mwalimu mkuu wa shule hiyo ndugu Benjamen Ngowi ambaye alieleza changamoto ya bweni kwa kueleza kuwa Halmashauri ilishapendekeza bajeti katika Mwaka mpya wa fedha juu ujenzi na ukarabati wa miundombinu ya kwa tarafa ya Ngorongoro.
“Sisi kama Halmashauri tulishaandaa mapendekezo ya bajeti na pindi itakapopitishwa basi bweni hilo litajengwa katika shule hii, na Rais wetu Mhe. Samia Suluhu Hassan ni msikivu na anawapenda Wananchi wake, pia nitoe Rai kwenu walimu muongeze ufanisi katika ufundishaji ili hali ya ufaulu wa kitaaluma uendelee kuongezeka”
Mhe Bayo ameahidi kuwa halmashauri itaendelelea kushirikiana na serikali ili kuhakikisha kuwa mahitaji ya wananchi yanatatuliwa kwa haraka. Wananchi walionyesha furaha na matumaini makubwa kutokana na ziara hiyo, wakiamini kuwa hatua hizo zitachangia katika kuboresha maisha yao siku za usoni.
Ziara hii ni sehemu ya juhudi za halmashauri ya wilaya ya Ngorongoro katika kuhakikisha kuwa maendeleo yanapatikana kwa ushirikiano wa karibu kati ya viongozi na jamii. Wananchi wamesisitiza umuhimu wa kuendelea kushirikiana na viongozi wao ili kufanikisha malengo ya maendeleo endelevu.