Mikopo yenye thamani ya milioni 261 yatolewa kwa vikundi Ngorongoro
6 December 2024, 3:41 pm
Katika kuhakikisha utekelezaji wa mpango wa Serikali wa kutoa asilimia kumi ya mapato ya ndani ya halmashauri kwa makundi maalum halmashauri ya Ngorongoro imekabithi kwa vikundi hivyo mikopo hiyo kwa lengo ya kujikwamua kiuchumu.
Na mwandishi wetu
Mkuu wa Wilaya ya Ngorongoro, Kanali Wilson Sakulo, amekabidhi mikopo yenye thamani ya shilingi milioni 261 kwa vikundi 45 vya wanawake, vijana, na watu wenye ulemavu katika hafla iliyofanyika hii leo, Desemba 6, 2024, katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri ya Wilaya ya Ngorongoro. Hafla hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa mpango wa Serikali wa kutoa asilimia kumi ya mapato ya ndani ya halmashauri kwa makundi haya maalum.
Akizungumza katika hafla hiyo, Kanali Sakulo aliwataka wanufaika kutumia mikopo hiyo kwa busara, ili iwe chachu ya maendeleo kwao binafsi, familia zao, na jamii kwa ujumla. Alisisitiza kuwa mikopo hiyo siyo ya matumizi yasiyofaa kama kununua nguo, kufanya mitoko, au kuongeza wake au waume, bali ni fursa ya kuboresha maisha na kujenga heshima katika jamii.
Kwa upande wake, Kaimu Afisa Maendeleo ya Jamii wa wilaya hiyo, Bw. Burhan Kayumba, alieleza kuwa mikopo hiyo imetolewa kwa mujibu wa sheria na imegawanywa kama ifuatavyo,Vikundi 17 vya wanawake vilipokea mikopo yenye thamani ya shilingi milioni 101.Vikundi 24 vya vijana vilipokea mikopo yenye thamani ya shilingi milioni 142.Vikundi 4 vya watu wenye ulemavu vilipokea mikopo yenye thamani ya shilingi milioni 18.
Bw. Noel Kasone, mwakilishi wa Kikundi cha Faraja kutoka kijiji cha Digodigo, alimshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuruhusu mpango huu wa mikopo ya asilimia kumi. Aliahidi kuwa kikundi chao kitaitumia mikopo hiyo kwa shughuli za gereji, wakilenga kuongeza ufanisi na mapato.
Kwa mujibu wa kanuni za mikopo hiyo, kila kikundi kinatakiwa kuanza kurejesha mkopo baada ya miezi mitatu, kwa awamu za kila mwezi, kulingana na makubaliano kati ya vikundi na Mamlaka ya Serikali za Mitaa.