Loliondo FM

Ngorongoro wamshukuru rais Samia kwa kuruhusu kushiriki uchaguzi

19 October 2024, 12:42 pm

Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Ngorongoro mh Marekani Mohamed Bayo

Wilaya ya Ngorongoro inaunguna na wilaya zingine nchi nzima katika zoezi la uandikishaji wa wapiga kura kuelekea uchaguzi wa serikali za mitaa huku idadi ya wananchi waliojitokeza kuandikishwa hadi hivi Sasa ikiwa na ya kuridhisha.

Na mwandishi wetu.

Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Ngorongoro mhe. Marekani Mohamed Bayo amemshukuru rais wa jamhuri ya muungano wa Tanzania Mhe.Samia Suluhu Hasani kwa kufuta tangazo lililokua linazuia wananchi wa tarafa ya Ngorongoro kushiriki katika zoezi la uchaguzi wa serikali za mitaa.

Ameyasema hayo Oktoba 18 2024 wakati akifungua mkutano wa baraza la madiwani kwa robo ya kwanza ya mwaka wa fedha 2024/2025 yani Julai – Novemba ambapo amewahakikishia wakaazi wa tarafa na wilaya ya Ngorongoro kwa ujumla kua halmashauri imeweka mikakati ya utekelezaji wa shughuli za maendeleo kwa kubadilisha matumizi baadhi ya fedha kutoka katika miradi mingine ili kuleta maendeleo na kupunguza umasikini katika tarafa hio ambayo imetatizika kutekelezwa mirandi ya maendeleo katika sekta za afya,elimu,miundombinu na mingine mingi kwa kipindi cha miaka minne.

Katika makusanyo kipindi cha Julai – Septemba halmashauri ya wilaya ya Ngorongoro imekusanya mapato kwa asilimia 32 ya makadirio ya kukusanya kiasi cha shilingi bilioni 3.58 kwa mwaka wa fedha 2024/25 kutoka katika vyanzo mbalimbali huku akiwataka wataalam wa halmashauri kutobweteka na mafanikio hayo ya makusanyo wafanye kazi kwa bidii ili kufikia lengo la makusanyo la mwaka ili kutekeleza kwa ukamilifu miradi ya maendeleo,kuinua wananchi kiuchumi pamoja na utekelezaji wa afua mbalimbali ikiwemo za lishe.

Halikadhalika ametolea tathmini juu ya zoezi linaloendelea la uandikishaji wapiga kura katika daftari la wapiga kura wakaazi ili kushiriki uchaguzi wa serikali za mitaa utakao fanyika Novemba 27 ambapo zaidi ya asilimia 95 ya malengo imeandikishwa huku akiwasihi madiwani kuhimiza wananchi katika kata zao kujiandikisha kwa wingi ili wasikose haki yao ya kupiga kura na kuwachagua viongozi wa kuwaletea maendeleo katika vijiji,vitongoji na mitaa yao.

Katika hatua nyingine baraza limetambua mchango unaotolewa na wahisani wa maendeleo na kujadili kwa kuweka maazimio matatu juu ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo inayotekelezwa kwa hisani kutoka shirika la benki ya maendeleo ya Ujerumani (kfw) na kuonyesha kutoridhishwa na muda mrefu wa utekelezaji wa miradi hio ,gharama kubwa ya ujenzi ikiwemo nyumba ya wawili kwa moja (2 in 1) inayojengwa kwa zaidi ya milioni mia mbili na ushirikishaji duni hasa wa uibuaji wa miradi yenyewe kutoka katika vijiji kunakotekelezwa miradi hiyo.