Watakiwa kufuata maelekezo ya serikali kuboresha huduma za kijamii Ngorongoro
12 September 2024, 7:41 pm
Inatajwa kuwa askari walio wengi wa hifadhi hapa nchini wamekuwa wakiingia migogoro na wananchi wanao zizunguka hifadhi kutona na sababu mbalimbali ikiwepo mifugo yao kuingia hifadhini.
Na mwandishi wetu.
Askari uhifadhi wa mamlaka ya hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) wametakiwa kujenga mahusiano mazuri na wananchi wanaozunguka hifadhi ya Ngorongoro ili kuendeleza juhudi za uhifadhi za eneo hilo.
Waziri wa maliasili na utalii, mhe. balozi, dkt. Pindi Chana (mb) ameyasema hayo leo Septemba 12, 2024 alipokuwa akizungumza na watumishi wa mamlaka ya hifadhi ya eneo la Ngorongoro katika makao makuu ya ofisi za NCAA wilayani Karatu mkoani Arusha.
“Tuendelee kuboresha mahusiano kati yetu na wananchi na kuwasikiliza wanapokuwa na maoni au changamoto kwa sababu watatusaidia katika mipango yetu ya uhifadhi” amesisitiza mhe. Chana.
Aidha, amewataka kuendelea kufuata maelekezo mbalimbali ya serikali ikiwa ni pamoja na kuboresha utoaji wa huduma za kijamii kwa wananchi kama geti na vyoo vya wanafunzi.
Amewataka kufanya kazi kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu zilizopo kwa kuwa mheshimiwa rais dkt. Samia Suluhu Hassan ana imani kubwa na NCAA katika kutoa huduma, kukusanya mapato na kuendeleza uhifadhi.
Pia amewataka kuwa wazalendo na kusimamia vizuri zoezi la kuhama kwa hiari ili zoezi liende vizuri.
Naye, katibu mkuu wizara ya maliasili na utalii, dkt. Hassan Abbasi amesema hifadhi hiyo imeongeza idadi ya watalii kwa asilimia 21 kwa takwimu za mwezi Januari hadi Juni, 2024 watalii wa nje walikuwa 180,000 mpaka 200,000 na zaidi huku akisisitiza kuwa wizara imeendelea kutimiza wajibu wake katika kuisimamia NCAA.
Ameweka bayana kuwa pamoja na mafanikio hayo mh rais amefanya azimio kubwa la kutoa asilimia 3 ya mapato kwa ajili ya uhifadhi na asilimia 6 kwa ajili ya kutangaza utalii.
Mapema akizungumza katika kikao hicho kamishna wa uhifadhi wa mamlaka ya hifadhi ya Ngorongoro, dkt. Elirehema Doriye ameipongeza wizara ya maliasili na utalii kwa kuendelea kusimamia vizuri kazi mbalimbali za mamlaka hiyo.