Waandishi wa habari waaswa kufanya kazi kwa maslahi ya wananchi
23 August 2024, 1:17 pm
Kufuatia yanayoendelea Ngorongoro na kuelekea Uchaguzi wa serikali za mitaa maratibu wa THRDC awataka Waandishi wa habari wasikae kimya kwa sababu wananchi wanaumia.
Na Saitoti Saringe
Akizingumza hii leo Agosti 23, 2024 jijini Dodoma akifungua mafunzo kwa Waandishi wa Habari kutoka vyombo mbalimbali nchini, Wakili Olengurumwa amesema kuwa vyombo vya habari ni muhimu katika kuwasaidia wananchi kuweza kuibua matatizo yao na kuzipeleka kwenye mamlaka husika.
“Vyombo vya habari msaidie kuripoti habari za jamii ili kuwasaidia wananchi, mfano kule Ngorongoro kuna vyombo vya habari hazijaripoti yanayoendelea ni kama hawajui kinachoendelea ni vyombo vichache sana vinaripoti habari hizo, wananchi wenyewe wanaripoti taarifa kwa simu zao hakuna chombo chochote cha habari kule’- Olengurumwa
Aidha Olengurumwa amesema kuwa Mafunzo hayo yalioandaliwa na THRDC yanalenga kuwajengea uwezo waandishi wa habari kuripoti habari za uchaguzi kuelekea Uchaguzi wa serikali za mitaa na uchaguzi mkuu ujao 2025.
Katika Hutua nyingine Olengurumwa amewaasa waandishi wa habari kutojihusisha au kufungamana na vyama vya siasa nchini wakati wa uchaguzi ili isiadhiri kazi zao na kushindwa kufanya kazi zao ipasavyo.
Mafunzo hayo yanayotarajiwa kufanyika kwa siku mbili jijini Dodoma imehusisha waandishi wa habari takribani 50 kutoka katika vyombo mbalimbali hapa nchini.