Mhitimu kidato cha sita Loliondo afariki kwa kupigwa risasi kwenye maandamano
23 August 2024, 12:23 am
Ni maandamano yaliyofanyika Agosti 21, 2024 mkoani Simiyu kwa wananchi kuandamana wakidai polisi kutochukua hatua ya kufuatilia matukio ya kupotea kwa watoto na kupatikana wakiwa wamefariki dunia.
Na mwandishi wetu.
Kijana Meshack Daudi Paka (21) mhitimu wa kidato cha sita shule ya sekondari Loliondo mkoani Arusha amefariki dunia kwa kupigwa risasi wakati polisi wakiwatawanya wananchi waliofanya maandamano Lamadi wilaya ya Busega mkoani Simiyu.
Lengo la maandamano hayo yaliyofanyika mapema Agosti 21,2024 limetajwa kuwa ni kuishinikiza serikali ya mkoa kuingilia kati na kutafuta suluhisho la matukio yaliyojitokeza mara kwa mara ya watoto kutekwa au kupotea ambayo waliwalaumu polisi kutochukua hatua za kuridhisha.
Akizungumza kwa uchungu mama wa kijana huyo ameeleza namna alivyoagana na mwanae Meshack na jinsi alivyopokea taarifa za mwanae kupigwa risasi.
Ameongeza kuwa mwanae alikuwa anategemewa kwenda chuo baada ya kumaliza kidato cha sita huku hakiwaomba wananchi kutojichukulia sheria mkononi hususani kuandamana kwani sababu ya kifo chamwanae ni maandamano.
Kwa upande wake baba wa mtoto huyo Bw Daudi Paka ameeleza kusikitishwa na tukio la kupigwa risasi kwa mwanae na namna ambavyo maandano hayo yalivyoanza hadi mwanae kupigwa risasi ya tumboni.
Sambamba na hayo ameeleza namna alivyopokea taarifa za mwanae kupigwa risasi huku hakiekeza namna ambavyo mtoto huyo alivyokuwa anafanya vizuri katika masomo yake na kuiomba serikali kutotumia nguvu kubwa katika swala la maandamano kuwatuliza wananchi.
Mkuu wa mkoa wa Simiyu Kenan Kihongosi amesema jana katika mkoa walipata changamoto wananchi walifanya maandamano baada ya watoto wawili kupotea, wananchi waliandamana wakati uchunguzi ukiwa unaendelea wakafunga barabara, vurugu zikaendelea kwa kurusha mawe kwa vyombo vya usafiri hali ambayo ilikua inahatarisha pia usalama wa wasafiri jambo ambalo liliwalazimu polisi kutumia mabomu ya machozi kutuliza ghasia lakini haikuweza kusaidia mwisho wa siku polisi ikawajeruhi wananchi wanne ambao watatu walikuwa majeruhi ilipofika majira ya saa mbili walipata taarifa kwamba kuna mwananchi mmoja amefariki na kuwasiliana na jeshi la polisi na wakathibitisha ni kweli.