Loliondo FM

367 wahamia Msomera licha ya maandamano Ngorongoro

22 August 2024, 9:33 am

Kundi la wananchi waliokubali kuhama kutoka Ngorongoro kuelekea Msomera (picha na NCAA)

Kumekuwa na maandamano kwa wananchi wanaoishi tarafa ya Ngorongoro wakiitaka serikali kuwasikiliza na kutatua changamoto na kero zinazowakabili bila ya mafanikio, hata hivyo wengine wameendelea kukubali kuhama kwa hiari kulekea Msomera.

Na mwandishi wetu.

Mwitikio wa wananchi wanaoishi katika eneo la hifadhi ya Ngorongoro kuendelea kuhama kwa hiari umepamba moto licha ya uwepo wa maandamano katika eneo hilo ambapo leo tarehe 22 Agosti, 2024 jumla ya kaya 79 zenye watu 367 na mifugo 995 zimehama kutoka hifadhi ya Ngorongoro kwenda Kijiji cha Msomera Handeni na maeneo mengine waliyochagua wenyewe.

Akiwaaga wananchi hao naibu katibu mkuu wa wizara ya maliasili na utalii (anayesimamia maliasili) CP Benedict Wakulyamba amesema kuwa kuondoka kwa kundi hilo leo ni sehemu ya utekelezaji wa mpango wa kulinusuru eneo la hifadhi ya Ngorongoro ambapo wananchi wameendelea kuelimishwa na kuhama kwa hiari kwa ajili ya kuboresha maisha yao na kunufaika na fursa za kiuchumi zilizoko nje ya hifadhi.

Ametoa tahadhari kuwa wapo baadhi ya wananchi ambao wamekuwa wakihamia Msomera kinyemela bila kufuata utaratibu uliowekwa na kuleta changamoto kwa ndugu zao wanaowakuta huko na kuwasihi kuwa kufuata utaratibu na miongozo iliyowekwa ili wawe wakazi halali wa maeneo wanayopenda kuhamia.

Akitoa taarifa ya utekelezaji wa mpango wa kuhamisha wananchi wa Ngorongoro kwa hiari, afisa uhifadhi mkuu na meneja mradi wa kuhamisha wananchi kwa hiari PCO Flora Assey amebainisha kuwa tangu zoezi hilo lilipoanza mwezi Juni, 2022 hadi kufikia mwezi Agosti, 2024 takriban kaya 1,598 zenye watu 9,618 na mifugo 39,779 imeshahama ndani ya hifadhi kwenda kijiji cha Msomera na maeneo mengine.

Akiongea kwa niaba ya kamishna wa uhifadhi, kamishna msaidizi mwandamizi wa uhifadhi mhandisi Daniel Chegere ameeleza kuwa NCAA inaendelea na zoezi la kuwaelimisha wananchi kuhusu umuhimu wa kuhama kwa hiari katika eneo la hifadhi na kwenda maeneo yaliyotengwa na Serikali kwa kujengewa miundombinu ya kisasa yenye huduma zote muhimu za kijamii ambazo ni salama zaidi tofauti na ilivyo ndani ya ya hifadhi.

Mhandisi Chegere ameongeza kuwa hali ya usalama katika hifadhi hiyo inaendelea vizuri, ambapo ulinzi umeimarishwa na wageni mbalimbali wanaotembelea hifadhi hiyo wanaendelea na shughuli za utalii bila changamoto.

Huku hayo yakiendelea kumekuwepo na maandamano katika eneo hilo la Ngorongoro na hadi hivi Sasa hakuna tamko ramsi la serikali kuhusu maandamano hayo.