Mabeyo aagiza maboresho magofu ya Engaruka
10 August 2024, 4:35 am
Magofu ya Engaruka ni moja ya maeneo yenye historia kubwa sana Tanzania miaka 500 hivi iliyopita, jamii ya wakulima ilitumia mfumo wa hali ya juu wa kilimo cha umwagiliaji katika eneo hilo.
Na Mwandishi wetu.
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Mamlaka ya Hifadhi ya Eneo la Ngorongoro (NCAA) Jenerali Venance Mabeyo (mstaafu) ameuelekeza uongozi wa mamlaka hiyo kuweka jitihada za kuboresha miundombinu katika kituo cha magofu ya Engaruka kilichosheheni historia ya teknolojia ya kilimo cha umwagiliaji kilichofanyika eneo hilo karne ya 14 hadi 18.
Jen. Mabeyo ameyasema hayo Agosti 8, 2024 akiwa katika ziara yake ya kikazi wilayani Monduli mkoani Arusha katika magofu hayo ya Engaruka.
Akiwa na wakurugenzi wa bodi ya NCAA, Jenerali Mabeyo ameeleza kuwa eneo hilo lililopo pembezoni mwa hifadhi ya Ngorongoro ni miongoni mwa vituo vya malikale vinavyosimamiwa na NCAA ambapo historia inaonesha wakazi walioishi Engaruka karne ya 14 walitumia eneo hilo kwa shughuli za kilimo cha mazao mbalimbali yaliyostawi kutokana na uwepo wa maji ya kutosha yanayotiririka muda wote kutoka msitu wa Nyanda za Juu Kaskazini katika hifadhi ya Ngorongoro.
Mkuu wa kituo cha magofu ya Engaruka Bw. Jackson Tito ameueleza ujumbe wa wakurugenzi wa bodi ya NCAA kuwa, wageni wanaotembelea eneo hilo wanapata fursa ya kujua teknoloijia ya umwagiliaji kuanzia maandalizi ya mashamba, mifereji ya maji kwa ajili ya umwagiliaji, kuona masalia ya vyungu vya kupikia na mafiga yake na zana zingine za kale zilizotumiwa na jamii iliyoishi katika eneo hilo.
Teknolojia hii inahusishwa na jamii ya wairaq na wasonjo walioishi katika eneo la Engaruka katika karne hizo.