Ujenzi wa nyumba Msomera wafikia asilimia zaidi ya 90
9 July 2024, 12:15 am
Katika juhudi za kuendelea kuboresha mazingira na kujenga nyumba za kutosha katika kijiji cha Msomera ili kuwezesha wananchi watakao hama kwa hiari kutoka hifadhi ya Ngorongoro wanapata sehemu nzuri yakuishi pamoja na mifugo yao sasa ujenzi wa nyumba umekamilika ni zaidi ya asilimia 90.
Na mwandishi wetu.
Katibu Mkuu wa wizara ya maliasili na utalii Dkt Hassan Abbasi amelipongeza jeshi la kujenga taifa kupitia kampuni yake ya SUMA-JKT kwa kufikia zaidi ya asilimia 90 kukamilisha ujenzi wa nyumba 2,500 zinazojengwa katika kijiji cha Msomera wilayani Handeni mkoani Tanga.
Dkt Abbasi ametoa kauli hiyo katika ziara aliyoifanya kijijini hapo Julai 8, 2024 na kusema kazi iliyofanywa na jeshi hilo ni kubwa na ya kizalendo hivyo zoezi lililobaki sasa ni kuendelea kuelimisha, kuhamasisha na kuhamisha wananchi wanaoendelea kujiandikisha kuhama kwa hiyari katika eneo la tarafa ya Ngorongoro.
Amesema kuwa ujenzi wa nyumba hizo unaenda sambamba na ujenzi wa miundombinu mingine ya huduma za kijamii ambapo wizara za kisekta zimekuwa zikiendelea kujenga miundo mbinu hiyo ikiwemo shule,usambazaji wa umeme,maji ,mawasiliano na huduma zote za msingi katika kijiji hicho.
Naye kanali Sadiki Mihayo mkuu wa operesheni kutoka Suma Jkt amesema hadi sasa mradi huu amefikia asilimia 90 katika nyumba zote 2500 zaidi ya nyumba 2350 tayari zimekishwa kamilika na zipo tayari kwa wananchi wanaohama kwa hiari kutoka Ngorongoro.
Kwa upande wake mkuu wa wilaya ya Handeni mheshimiwa Albert Msando amemshukuru Dkt Abbasi kwa ziara hiyo na kusema kuwa itaongeza ari kwa wizara nyingine za kisekta kuongeza kasi katika ukamilishaji wa miradi yote muhimu na hivyo kuifanya Msomera kuwa kijiji cha mfano.
Mheshimiwa Msando amesema kuwa uendelevu wa mradi huo unaondoa propaganda za watu wachache kwamba wananchi wanaohamishwa kutoka Ngorongoro kwenda katika kijiji hicho wanaondolewa kwa nguvu na kutelekezwa jambo ambalo halina ukweli wowote.
Kuhusu suala la kuhamisha watu kwa hiyari kutoka ndani ya hifadhi ya Ngorongoro kamishna wa mamlaka ya uhifadhi ya Ngorongoro (NCAA) Dkt. Elirehema Doriye amesema kukamilika kwa nyumba hizo kunaongeza chachu ya mamlaka kuendelea kuhamasisha na kuhamisha wananchi.