Loliondo FM

Mtumishi wa afya akamatwa akiuza dawa na vifaa tiba mnadani Ngorongoro

3 July 2024, 7:54 pm

Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Ngorongoro bwn Murtallah Sadiki (picha na mpiga picha wetu)

Serikali imekuwa mstari wa mbele kwa kuhakikisha wananchi wake wanapata huduma bora za afya kwa kununua vifaa tiba na dawa kwa fedha nyingi lakini baadhi ya watumishi wa afya wameshindwa kuzingatia maadili ya utendaji wao wa kazi kwa kiviuza kwa malengo yao binafsi.

Na Edward Shao

Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Ngorongoro Bw Murtallah Sadiki amemsimamisha kazi tabibu msaidizi zahanati ya Orimanie dr Samweli Panga kwa tuhuma za kukamatwa na dawa na vifaa tiba akiwa anaviuza katika mnada wa Olbalbal tarafa ya Ngorongoro kinyume na taratibu na kanuni za utumishi.

Akizungumza kusimamishwa kazi kwa mtumishi huyo hii leo Julai 03 ,2024 huyo bw Murtallah Sadiki amesema mtumishi huyo alihamishwa kutoka zahanati ya Misigio tarafa ya Ngorongoro kuelekea zahanati ya Orimanie na baada ya kuripoti kituo chake cha kazi aliomba kwenda kufuata mizigo yake lakini akurejea tena kituoni akishinikiza kulipwa fedha zake za uhamisho licha ya kuandaliwa gari ya kuisafirisha familia yake.

Amesema baada ya kutorudi kazini walipewa taarifa kuhusu mtumishi huyo kufanya mambo yasiyo mazuri hivyo waliweka mitego kwa kushirikina na diwani wa eneo hilo na hatimaye Juni 13,2024 alionekana akiwa na vifaa tiba hivyo kwenye boksi anapanda gari kuelekea mnadani kuviuza na alipohojiwa na jeshi la polisi alisema alikuwa anakwenda kliniki.

Sauti ya mkurugenzi

Kaimu mganga mkuu halmashauri ya wilaya ya Ngorongoro dr Libori Tarmo amekiri mtumishi huyo kukamatwa na dawa na vifaa tiba vyenye thamani ya shilingi 344,213.90 akiwa anaviuza mnadani huku akitoa wito kwa watumishi wengine kuacha tabia za kutumia vibaya dawa pamoja na vifaa tiba vilivyotolewa na serikali kwaajili ya matibabu kwa wananchi.

Sauti ya kaimu mganga mkuu

Kwa mujibu wa mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Ngorongoro ili iwe fundisho kwa wengine mtumishi huyo yuko mikononi mwa jeshi la polisi kwa taratibu nyingine ikiwepo kufikishwa mahakamani endapo atabainika kuhusika na wizi huo.