Dc Ngorongoro:Tatueni migogoro kwenye kata zenu
14 June 2024, 9:07 am
Na Zacharia James
Mkuu wa wilaya ya Ngorongoro Mhe.kanali Wilson Sakulo amewataka waheshimiwa madiwani kushiriki kikamilifu kusaidia kutatua migogoro yote iliyopo katika maeneo ya kata zao kwani wao wananguvu kubwa na imani ya Wananchi wao.
Ameyasema hayo katika mkutano wa baraza la halmashauri kwa robo ya tatu ya mwaka 2024 kilichofanyika Juni 13, 2024 katika ukumbi wa halmashauri ya Ngorongoro ambapo amechukua nafasi hio kuwapongeza madiwani wa kata za Oloipiri na Soitsambu ambao wameweka juhudi za makusudi kumaliza mgogoro wa mpaka kati yao kwa kushirikiana na viongozi wa mila na amewahakikishia wakimaliza ataishauri Sekta ya ardhi wilaya kupitisha mipaka itakayo kubaliwa.
Mhe. Sakulo amewasihi waheshimiwa madiwani kuwahamasisha Wananchi katika kata zao kushiriki kikamilifu katika zoezi la maboresho ya daftari la kudumu la wapiga kura, zoezi ambalo ameeleza mchakato na taratibu zake zitaanza tarehe 1 Julai, 2024 ili kuhakikisha kwamba ifikapo wakati wa kupiga kura watekeleze haki yao ya kikatiba kwa kuchagua viongozi huku pia akichukua nafasi hio kuipongeza halmashauri ya wilaya ya Ngorongoro kuongeza makusanyo ya mapato.
Kwa upande wake mwenyekiti wa halmashauri ya wiilaya ya Ngorongoro Mhe. Mohamed Bayo amesema katika kipindi cha mwezi Mei halmashauri imekusanya kiasi cha sh.178,786,931 na kufanya jumla ya makusanyo kuwa shilingi 2,586,714,284, sawa na 83% ya makisio ya kukusanya jumla ya shilingi 3,101,200,000.
Sambamba na hayo ametoa rai kwa mkurugenzi wa hamashauri ya Ngorongoro kupitia divisheni ya mipango ikutane na wenyeviti wa kata na vijiji ili kushughulikia vifungu katika mfumo mpya wa manunuzi inayosababisha vijiji kushindwa kutumia fedha zilizopo katika akaunti zao.
Hata hivyo amegusia suala la njia za ukusanyaji mapato amebainisha kua ofisi ya mkurugenzi ndio inayofanya ukusanyaji wa mapato hasa katika minada na sio vyombo vya usalama kama inavyopotoshwa kwani kamati ya fedha katika kikao chake cha mwisho kilichoketi mwezi wa nne kiliridhia kikosi kazi kilichoundwa kikihusisha kamati ya usalama kiendelee kusaidia kwenye ukusanyaji wa mapato.