Loliondo FM

Kamati: Kituo cha afya Arash kifanye kazi kabla ya Mei 20 Ngorongoro

17 May 2024, 10:33 am

Kamati ya fedha wilaya ya Ngorongoro wakitafakari jambo wakati ziara yao ya ukaguzi wa miradi ya maendeleo wilayani hapa, picha na mpiga picha wetu.

Wilaya ya Ngorongoro kupitia kamati yake ya fedha wamepanga ziara maalum za kukagua na kuhakikisha miradi mbalimbali ya maendeleo inayoendelea kutekelezwa wilayani hapa inatekelezwa kwa ubora na ufanisi wa hali ya juu.

Na mwandishi wetu.

Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Ngorongoro Mh. Mohammed Bayo ameiongoza kamati ya fedha, uongozi na mipango ya halmashauri katika ziara ya kutembelea na kukagua miradi ya maendeleo Mei 16 2024, inayoendelea kutekelezwa na serikali ya awamu ya sita chini ya usimamizi wa uongozi wa halmashauri.

Kamati imetembelea na kukagua jumla ya miradi mitatu ikiwemo ujenzi wa vyumba vya madarasa mawili na matundu ya vyoo nane katika shule ya sekondari Arash, kituo cha afya Arash na zahanati ya Ormanie.

Aidha, kamati hiyo imetoa ushauri wa kuongeza kasi ya shughuli ya ujenzi na kutoa rai kwa kaimu mganga mkuu wa wilaya kuhakikisha kituo cha afya cha Arash kinaanza kufanya kazi kabla ya tarehe 20 Mei, kwani miundombinu yote ya muhimu imeshakamilika na kutoa ahadi ya kurejea tena katika Kituo hicho tarehe 25 Mei, 2024 ili kuona namna huduma zinavyotolewa.

Ziara hiyo imeanza tarehe 15 Mei, 2024 na inatarajiwa kukamilika siku ya tarehe 17 Mei huku ikijumuisha timu ya wataalamu kutoka halmashauri ikiongozwa na mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Ngorongoro Bw. Murtallah Sadiki Mbillu.