Kamishna wa uhifadhi atumia milioni 400 kulala hotelini Ngorongoro
6 April 2024, 12:26 pm
Viongozi wa ngazi za chini waliochaguliwa na wananchi kutetea na kuibua kero zao wilayani Ngorongoro wameendelea kusimama na wananchi, hii ni baada ya diwani wa kata ya Alaitole tarafa ya Ngorongoro kuibua sakata la aliyekuwa kamishna wa mamlaka ya huifadhi ya Ngorongoro kutumia milioni 400 kulala hotelini kwa miezi mitatu.
Na Edward Shao.
Diwani wa kata ya Alaitole tarafa ya Ngorongoro mh James Moringe amedai kuwa aliyekuwa kamishna wa mamlaka ya hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) ndg Richard Kiiza alitumia shilingi milioni 400 ndani ya miezi mitatu kulala hotelini huku akigoma kuishi katika nyumba aliyokuwa ametengewa.
Mh Moringe amesema ndg Kiiza ambaye hata hivyo alikwisha ondolewa kwenye nafasi hiyo na mh Rais wa jamhuri ya muungano wa Tanzania Dr Samia Suluhu Hassan Machi 15,2024 alikuwa akilipa shilingi milioni 3.2 kama gharama ya hoteli kwa siku tangu kuteuliwa kwake tarehe 2/10/2023.
Hata hivyo wizara ya maliasili na utalii kupitia taarifa waliyoitoa wamesema walikuwa wamekwishaanza kufuatilia taarifa izo hata kabla ya diwani huyo kuzungumza na waandishi wa habari juu ya tuhuma hizo kwa ndg Kiiza.