RC Songwe awatahadharisha wazazi wanaowaozesha wanafunzi
May 9, 2024, 7:29 am
Na Denis Sinkonde,Songwe
Katika kupambana na vitendo vya ukatili wa kijinsia ikiwemo ndoa na mimba za utotoni, Mkuu wa Mkoa wa Songwe Daniel Chongolo, ametoa tahadhari kwa wazazi na walezi pamoja na wananchi kwa ujumla wilayani Ileje, mkoani humo wanaoendekeza vitendo vya kufungisha ndoa mabinti wenye umri mdogo, wakiwemo wanafunzi hali ambayo imekuwa chanzo cha mabinti wengi kukatisha masomo.
Akizungumza na wananchi wa Kata ya Ikinga, wilayani humo katika moja ya mkutano wake, Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Daniel Chongolo, amesema katika kukomesha vitendo hivyo ambavyo vimekithiri mkoani hapa.
Chongolo amesema serikali haitawafumbia macho watu wote wanaondekeza vitendo hivyo “Tukikubaini ulishiriki kula ule wali pale kwenye ile shughuli na wewe umeshiriki yule mtoto kuharibiwa, kwa hiyo tutasomba wote.
Serikali inatoa fedha kuboresha miundombinu ya shule ili watoto wasome lakini wanaharibiwa ndoto na wazazi na walezi kwa kuwaozesha wote tutawakamata pamoja na watakaohudhuria harusi tutakamata wote,” amesema Chongolo.