Triple A FM

Medali zaidi zinakuja-Simbu

30 September 2025, 11:58 am

Bingwa wa dunia wa Marathoni Alphonce Simbu akitua kwenye uwanja wa ndege wa Arusha Sept 29-2025

“Tuendelee kuwa Pamoja tushikamane tushirikiane tupendane na tuweze kusonga mbele”

Na Joel Headman

Bingwa wa dunia wa marathoni Mtanzania Alphonce Simbu baada ya mapokezi ya kishindo jiji Arusha ameahidi kupambana na kutafuta medali nyingine kwa ajili ya kulitangaza zaidi taifa kwenye michezo

Simbu alitua uwanja wa ndege wa Arusha majira ya mchana na kulakiwa na umati mkubwa wa watu uliojumuisha wanariadha,familia na maafisa wa jeshi la wananchi wa Tanzania ambalo naye ni mtumishi

Baada ya kuwasili alielekea pamoja na maeneo mengine kwenye uwanja wa mpira wa miguu wa Sheikh Amri Abeid sehemu ambayo huwa anafanya mazoezi

Bingwa wa dunia wa Marathoni Alphonce Simbu baada ya kuwasili jijini Arusha

Simbu Alitwaa medali ya Dhahabu katika mashindano makubwa zaidi ya riadha duniani (Tokyo 2025) yaliyofanyika nchini Japan Sept 15 na yenye ushindani mkali ikimlazimu kushinda sekunde 3 za mwisho mbele ya Mjerumani Amanal Petros akitumia muda wa masaa 2:09:48 Medali hiyo ni ya kwanza kwa Tanzania kwenye mashindano makubwa ya riadha duniani ambapo Tanzania imeondoka na medali 1 tu huku Kenya wakiongoza kwa Afrika kwa kutwa medali 11,Botwana 3 na mataifa mengine kama Afrika ya Kusini,Moroko na Nigeria wakirudi na medali moja moja