Triple A FM
Triple A FM
18 September 2025, 5:34 pm

Na Joel Headman
Wazee wa Kikombe cha bati, chai ya moto leo wamekiona cha moto kutoka kwa Purple Nation Mbeya City kwenye mchezo wa 3 wa ligi kuu uliomalizika jioni hii hapa Tanzanite Kwaraa Babati
Kipute hicho kilianza majira ya saa 8 mchana kwa kasi kubwa, kikishuhudia Fountain Gate wakiipelekea moto kwelikweli Mbeya City bila mafanikio mpaka kipindi cha kwanza kinamalizika wakiwa wamepiga mashuti 2 tu langoni kwa mkongwe Beno Kakolanya na mengine 5 yakienda nje
Kipindi cha pili kilianza vile vile kama cha kwanza lakini mashambulizi yakawa kwa zamu na kunako dakika ya 54 Mchezaji Shaaban Pandu alimfanyia madhambi Habib Kyombo wa Mbeya City ndani ya 18 na mwamuzi wa kati Abel Willium akaamuru pigo huru la penalty ambalo lilikwamishwa kimiani na Habib Kyombo dakika 56
Mabadiliko matatu yaliyofanywa na Mbeya City yalionekana kuwaelemea Fountain Gate iliyokuwa na wachezaji wa 3 tu wa akiba (kipa akiwemo) na kuwafanya wapinzani wao kuutawala mchezo mpaka ukamalizika kwa goli 1 kwa sifuri
Kocha wa Fountain Gate Denis Kitambi amesifu bidii za wachezaji wake na kukiri kuwa bado wana kazi ya kufanya kurekembisha makosa yaliyojitokeza wakati wakisubiri utawala kushughulikia mambo yaliyokwamisha wachezaji wengine kucheza
Kwa upande wake Mwalimu wa Mbeya City Malale Hamsini akijivunia majina ya wachezaji wake na uzoefu wao kwenye ligi ameshukuru kwa kile kilichofanyika na kueleza kuwa bado wana kazi zaidi ya kufanya
Timu zote 2 zitakuwa ugenini raundi ya 2 ya ligi kuu ambapo Mbeya City watakuwa wageni wa Azam na Fountain wakialikwa na Simba SC
Kocha wa Fountain amesema wataandaa mbinu kabambe za kumkabili mnyama na miongoni mwa hizo ni kumtazama kwa makini wikiendi hii akipepetuana na Gaborone United ya Botswana kwenye michuano ya CAF