Triple A FM
Triple A FM
16 August 2025, 6:36 pm

Na Joel Headman
Kampuni ya bia ya Tanzania Breweries PLC (TBL) imekusudia kuwainua zaidi wakulima wa Shayiri walioko kanda ya Kaskazini na maeneo mengine ya nchi ili kuongeza uzalishaji wa bidhaa hiyo muhimu ambayo hutumiwa kama kimea kwenye uzalishaji wa vinywaji vyake
Akizungumza katika kijiji cha Imori kilichopo Monduli juu mkoani Arusha kwenye hafla iliyowakutanisha wakulima wasiopungua 200 kuadhimisha siku ya wakulima wa Shayiri, mkurugenzi wa masuala ya sheria na mahusiano wa TBL bi Neema Temba amesema imekuwa ni utamaduni wao kuwasaidia wakulima ili kuwepo kwa manufaa ya pande zote mbili
Bi Temba ameeleza kuwa lengo la kampuni ni kuchangia katika mabadiliko ya jumla ya familia kiuchumi na hivyo wataendelea kushirikiana na wakulima hata katika wakati kilimo kinakabiliwa na changamoto tofauti kama vile mabadiliko ya tabia nchi
Akizungumza mmoja wa wakulima hao mzee Songoyo Olematat Lukumay ameishukuru TBL kwa kuhamasisha jamii ya kifugaji kujihusisha na kilimo cha Shayiri kwani kimesaidia kubadilisha masisha yao

Hata hivyo mtaalamu wa kilimo kutoka TBL bw.Benson Sangale amewashauri wakulima kuzingatia elimu wanayopatiwa ili kuwasaidia kupata mazao bora yenye tija kwa kiwanda na wakulima wenyewe
Kwa upande wake katibu tawala wa wilaya ya Monduli Muhsin Kassim akimuwakilisha mkuu wa wilaya hiyo ameeleza kuwa wakulima wa Shayiri wanapaswa kuongeza uzalishaji wa bidhaa hiyo kutokana na uhitaji mkubwa wa soko kwani mpaka sasa Kanda ya Kaskazini inazalisha tani 110,000 huku Arusha pekee ikitoa zaidi ya tani elfu 45 za Shayiri
Kampuni ya TBL ndio wazalishaji na wasambazaji wakuu wa bidhaa bora za kileo ikiwemo Safari Lager,Kilimanjaro na Castle Lager miongoni mwa nyingine
