Triple A FM
Triple A FM
29 May 2025, 10:58 am

Na Joel Headman
Ikiwa imepita miaka 33 tangu kuasisiwa kwa Chama cha Demokrasia na Maendeleo CHADEMA na kuingia kwenye mfumo wa vyama vingi mwaka 1992, bado viongozi na wanachama wanaendelea kutambua mchango wa viongozi na waasisi wao
CHADEMA ilianzishwa Mei 28 mwaka 1992 na Mei 28, 2025 imetimiza miaka 33 huku kukiwa na viongozi kadhaa waliokiongoza chama hicho kikuu cha upinzani nchini
Wakati wa kuinadi kampeni yao wanayoiendesha ya No Reforms, No Election (Hakuna uchaguzi bila mabadiliko) iliyofika Mkoani Arusha Mei 28, Imeshuhudiwa viongozi mbalimbali wa chama na wanachama wakikusanyika kujadili pamoja na mambo mengine ajenda hiyo wanayoipigia chapuo kwa sasa wakishinikiza mabadiliko ya mifumo ya uchaguzi.
Akihutubia katika eneo la soko kuu jijini Arusha, katibu mkuu wa CHADEMA John Mnyika amewataka wafuasi wao kundelea na mshikamano licha ya kipindi wanachokipitia akiwaasa kutowasahau waasisi wa chama toka kilipoanzishwa.
Akitaja majina ya waasisi na viongozi walioongoza kabla ya uongozi wa sasa, alimtaja pia mwenyekiti mstaafu Freeman Mbowe hali iliyoibua shangwe na nderemo kwa wafuasi
Katika hatua nyingine makamu mwenyekiti wa chama hicho John Heche ameeleza kuwa kamati kuu ya chama hicho itakutana tena mwanzoni mwa mwezi Juni kujadili hatua ya msajili wa vyama vya siasa nchini kukifutia ruzuku CHADEMA akifananisha kuwa ni mpango wa kukidhoofisha.